Wednesday, 14 March 2018

CUF yakutana na IRI


Julius Mtatiro

Suleiman Kasei

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimekutana na Mkurugenzi Mwakilishi wa Taasisi ya Kimataifa ya International Republican (IRI), Peter Okong'o na kuzungumza kuhusu hali ya kisiasa nchini na umuhimu wa wadau wote kushirikiana kuhakikisha demokrasia ya Tanzania inalindwa. 

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya chama hicho, Julius Mtatiro katika taarifa yake aliyotoa kwa vyombo vya habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.

“Nimemweleza ndugu Okong'o kuwa, wao IRI wanaweza kuendelea na kazi ya kushauri vyama vya siasa, serikali, taasisi za kidemokrasia, lakini kwa kweli sisi viongozi wa vyama na watanzania ndiyo wenye jukumu la kupigania haki na mabadiliko ya kweli,” amesema. 

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa baada ya maelezo ya kutosha kutoka CUF, Okong'o amewahakikishia kuwa taasisi yao itaendelea na juhudi zake za kufanya kazi na serikali wadau na wote ili kujenga uwezekano wa  utangamano na mabadiliko yanayotakiwa na wananchi. 

“Nimemhakikishia kuwa CUF na viongozi wake wako imara na watatoa mchango wao kwa nchi yao bila kukata tamaa, maana mabadiliko hayataletwa kwenye sahani bila kupiganiwa na wadau,” amesema. 

Mtatiro ameongeza kuwa Okong'o yumo katika ziara maalum ya kuwatembelea wakuu wa vyama hapa nchini, taasisi za kiraia, taasisi za usimamizi wa uchaguzi (NEC na ZEC) na Serikali.

Amesema IRI ni taasisi isiyo ya Kiserikali na kisiasa lakini imejikita katika kushauri kuhusu uhuru na demokrasia duniani ikiwemo kusaidia vyama vya siasa ili viweze kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu mipango mbalimbali ambayo Serikali imeweka kuhusu wao.

No comments:

Post a Comment