Sunday, 25 March 2018

Dk Kalemani azindua kiwanda kipya cha mita za umemeDk. Medard Kaleman (aliyesimama) akizungumza baada ya kuwasili kiwandani hapo.

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, amezindua kiwanda kipya cha kutengeneza mita za umeme, Baobab Energy Sytems Tanzania, kilichopo eneo la Mbezi juu Dar es Salaam, kinachomilikiwa na Watanzania. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dk. Kalemani amesifu uwekezaji uliofanywa na watanzania hao, na kueleza wazi kwamba hiki ni kiwanda cha kwanza chenye teknolojia chanya inayolenga kusaidia Tanzania kuokoa gharama za ununuzi wa mita na vifaa vya umeme kutoka nje ya nchi.

Dk. Kalemani ameipa Tanesco miezi 3 kuhakikisha inasitisha ununuzi wa mita za umeme kutoka nje ya nchi kwani tayari viwanda vya ndani kikiwemo Baobab vimeonesha kuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa inayokidhi mahitaji ya nchi.

“Kwa sasa kiwanda kina uwezo wa kuzalisha mita za umeme 38,000 kwa mwezi, wakati mahitaji ya tanesco ni 20,000 kwa mwezi, hivyo naipa Tanesco miezi mitatu waangalie kazi inayofanywa na wataalamu hawa na waanze kununua mita hizo kutoka kwa wazalishaji wa ndani,” amesema.

Hadi sasa hapa nchini kuna viwanda viwili vya uzalishaji wa mita za umeme, Baobab kikiwa ni miongoni mwa viwanda hivyo.

Pia Waziri ameiagiza Tanesco kushirikiana na wazalishaji hao wa mita za umeme ili kupunguza ulazima wa kupeleka mita na vifaa kama hivi nje ya nchi kwa ajili ya matengenezo pindi vinapoharibika.

Mkurugezi mkuu wa Baobab Energy Systems Tanzania, Mhandisi Hashim Ibrahim amesema wamewekeza katika uzalishaji huo wa mita za umeme, kwani wameona changamoto kubwa inayoipata serikali ya kuagiza mita kutoka nchi nyingine.

Ibrahim amesema licha ya mambo mengine kiwanda hicho pia kitatoa ajira kwa vijana wa kitanzania hasa wanaohitimu vyuo mbalimbali hapa nchini vikiwemo vya Ufundi Stadi (Veta).

No comments:

Post a Comment