Tuesday, 20 March 2018

Dk Mwakyembe aahidi kufikisha taarifa za tafiti kumbukumbu kwa mawaziri wenzake


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesimama katika jukwaa ambalo Mwalimu Julius Nyerere alisimama kuhutubia wananchi lililopo katika Uwanja wa mikutano uliokuwa ukitumiwa naye kuendeshea mikutano, wakati wa ziara yake ya kutembelea maeneo ya urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika leo mkoa hapa.


Peter Simon, Mbeya


WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo,  Dk. Harrison Mwakyembe ameahidi kufikisha taarifa ya hatua ambayo Tanzania imefikia katika harakati za kutafiti na kuhifadhi kumbukumbu za ukombozi wa Bara la Afrika kwa mawaziri wa utamaduni wa nchi za Kusini mwa Afrika ili ziweze kuendelea na hatua nyingine ya kuchangia ujenzi wa kituo cha kuhifadhi kumbukumbu hizo.

Waziri Mwakyembe ameyasema hayo leo, mkoani Mbeya alipofanya ziara ya kukagua maeneo yaliyotumika wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na kuongeza kuwa serikali ipo katika mpango wa kuhifadhi maeneo yaliyotumika katika harakati za ukombozi wa bara hilo kwa kuyakarabati na kuyarejesha katika muonekano wake wa awali ili yasipotezi historia.

“Majengo yaliyotumika kwenye harakati za urithi wa ukombozi wa Bara la Afrika ni sehemu ya historia na ni maeneo muhimu sana ambayo yanatakiwa kuboreshwa ili yaweze kuendelea kuwepo katika muonekano ule ule wa awali tunafanya hivi ili kulinda historia yake,” amesema.

Aidha, Dk. Mwakyembe amesema serikali imetimiza wajibu wake wa kubaini maeneo yaliyotumika wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika na kuwaomba viongozi wote nchini kuendelea kubaini maeneo na vitu vilivyotumika katika harakati za ukombozi vilivyopo katika maeneo yao ili wizara iyaendeleze kwa maslahi ya taifa na Afrika kwa ujumla

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika ameitaka programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kuzingatia na kuchukua taarifa ya vitu mbalimbali kama vile vyakula vilivyotumika, vifaa na nyimbo  za kuhamasisha ukombozi wa bara hilo ili jamii ya sasa na ijayo ifahamu kumbukumbu hizo kwa undani zaidi.

Naye Mratibu wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, Ingiahedi Mduma amesema hadi sasa programu inakusanya vitu vyote vilivyotumika wakati wa harakati za ukombozi wa bara hilo ambapo nyimbo 42 zilizokuwa zikihamasisha mambo ya ukombozi zimekusanywa, hotuba 78 zilizotumika wakati wa harakati za ukombozi zimepatikana, maeneo 161 yaliyotumika wakati wa harakati za ukombozi yameainishwa na watu 201 wamehojiwa ambao kwa namna moja ama nyingine wamepitia harakati hizo.

Baadhi ya maeneo yaliyobainika mkoani Mbeya kutumiwa na wanaharakati na wapigania uhuru wa Bara la Afrika ni pamoja na Game, Nyumba ya Binti Matola, Nyumba ya Juma Mtoto, Uwanja wa Mikutano, Sekondari ya Samora Michel, Nyumba iliyopo Iyela iliyotumiwa na Samora Michel pamoja na Nyumba za kwa Mapunda.

No comments:

Post a Comment