Tuesday, 13 March 2018

Dk Ndugulile: Serikali inatambua umuhimu wa tiba asili


Dk Faustine Ndugulile

Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema inatambua umuhimu wa tiba asili na mbadala kwa kuwa ndiyo asili ya taifa kwa kuwa zilianza kutumiwa na mababu tangu kale.

Hali kadhalika amegiza Baraza la Tiba Asili na Mbadala kuacha kuwatoza tozo kubwa waganga wanaotaka kusajili dawa hizo kwa kuwa wengi wao kipato chao ni kidogo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile ametoa kauli hiyo leo, Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na wanahabari.

Pamoja na hilo, Dk. Ndugulile amewata watoa huduma hiyo kuzingatia vigezo ambavyo ni pamoja na kufuata sheria, kanuni na taratibu ikiwemo kujisajili wao, wasaidizi wao, vituo vya kutolea huduma na dawa zao.

Ametoa angalizo kwa waganga kuwa makini na baadhi ya vyama vya waganga vinavyojitangaza kuwasajili badala yake wajisajili Baraza la Tiba Asili na Mbadala.

“Serikali inawahamasisha waganga wa tiba asili kujiepusha na migongano katika jamii kutotumia ushirikina uchawi kama chanzo cha ugonjwa, shirikiane kupiga vita vitendo vinavyoharibu taaluma yenu ikiwemo mauaji ya vikongwe,”amesema Dk. Ndugulile.

Amewasisitiza waganga kubandika vyeti vyao vya usajili wa huduma wanazotoa katika eneo wanalotolea huduma ili kumwezesha mgonjwa kufahamu iwapo yeye amesajiliwa ama la.

Pia amewataka matabibu hao kutoa matangazo yanayoonesha sehemu ya kutolea huduma pamoja na mawasiliano, na si kueleza iwapo wao wanatibu maradhi gani.

Ametoa onyo pia kwa wale wanaouza dawa mbalimbali katika mabasi yanayokwenda mikoani nao wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa wanavunja taratibu.

Pia amelitaka baraza la tiba asili kuongeza wigo wa kutambua dawa asili na mbadala kwa kuweka utaratibu mzuri wa kusajili dawa na tozo ambazo zinaweza kugharamiwa na watoa tiba hizo.

No comments:

Post a Comment