Sunday, 25 March 2018

Donge nono kutolewa kwa atakayefichukua wanaong’oa alama za barabarani


Naibu Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa.

SERIKALI imetangaza kutoa zawadi nono kwa mwananchi atakayewezesha kupatikana taarifa za siri dhidi ya wanaong’oa alama za barabarani na kuisababishia hasara.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa mara baada ya kukagua ukarabati wa eneo Nyahua ambalo lilikuwa limekatika kutokana na maji ya mvua yaliyopelekea kukosekana kwa mawasiliano baina ya Itigi na Tabora, wilayani Uyui.

Amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuweka alama za barabara ili kuwaongoza watumiaji wa barabara kuepuka ajali lakini baadhi ya watu wamekuwa wakihujumu kwa kuzing’oa ili kwenda kuziua kama vyuma chakavu.

Kwandikwa amesema mtu atakayesaidia kutoa siri ya wanaong’oa alama hizo na wanunuzi wake atapewa zawadi na jina lake halitafichuliwa kwa ajili ya usalama wake.

Amesema inasikitisha kuona kuwa alama zipatazo 78 zenye thamani ya sh. milioni 27 katika kipande cha barabara ya urefu wa kilometa zipatazo 80.6 kutoka Tabora hadi Nyahua zimeng’olewa.

Naibu Waziri huyo amesema alama hizo zinatumia fedha nyingi za Serikali kwa kuwa baadhi yake zinatoka nje ya nchi na kuongeza kuwa vitendo hicho ni hatari hivyo ni vema wahusika wakikamatwa washitakiwe kama wahujumu uchumi.

Amesema hata pale Serikali ilipoamua kujengwa alama hizo kwa saruji bado baadhi ya watu wamekuwa wakizivunja ili kutoa nondo zilitumika katika ujenzi wake.

“Fikiria katika muda wa siku moja alama za barabarani 30 mkoani Kilimanjaro zimeng’olewa … Je? Kwa mwezi ni alama ngapi zinang’olewa ..fedha ngapi za Serikali zinapotea kurudisha alama hizo …Ma RC na Ma DC na wananchi saidieni kupambana na wahujumu wa miundombinu katika maeneo yenu” amesema Kwandikwa.

Aidha, Naibu waziri huyo amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wauzaji na wanunuzi wa vyuma chakavu watakao patikana na alama za barabara ili iwe fundisho kwa watu wanohujumu miundimbinu.

Kwandikwa amesema jamii inawajua vema wanaonunua vyuma chakavu ni vema wakatoa taarifa za siri ili kukomesha tatizo hilo ambalo limekuwa likichangia sehemu ya ajali nyingi za barabarani.

No comments:

Post a Comment