Tuesday, 20 March 2018

Faru pekee aliyesalia duniani afa Sudan


DUME la faru pekee aina ya Northern White Rhino aliyekuwa amesalia hai duniani, amekufa nchini Sudan  akiwa na umri wa  miaka 45, shirika la Ol Pejeta limetangaza.
Faru huyo alikuwa akitibiwa katika shamba kubwa la uhifadhi wanyama la kituo hicho kwa muda kutokana na matatizo yaliyotokana na kuzeeka kwake.
Alikuwa na vidonda visivyopona kutokana na umri wake. Shirika la Ol Pejeta limesema hali yake ilidhoofika zaidi katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
"Hakuweza hata kusimama na alikuwa anateseka sana," Ol Pejeta wamesema kupitia taarifa.Matabibu wa wanyama kutoka kituo cha uhifadhi wa wanyama cha Dvur Kralove, Ol Pejeta na Shirika la Wanyamapori Kenya waliamua kukatisha uhai wake.
Sudan ilikuwa maarufu sana duniani na ilikuwa nembo ya kutetea juhudi za kupigana na ujangili na kuwaokoa wanyama walio katika hatari ya kuangamia.
Alinusurika kuuawa porini alipohamishiwa katika kituo cha kuhifadhi wanyama cha Dvur Kralove miaka ya 1970.
Miaka ya baadaye, alirejeshwa Afrika na kuanza kutunzwa katika kituo cha Ol Pejeta.
Alichangia kuendeleza faru wa aina yake kwa kutungisha mimba faru wengine na kuchangia kuzaliwa kwa faru wengine wawili wa aina yake ambao sasa ndio pekee waliosalia hai.
Faru hao kwa jina Najin na Fatu ni majike, lakini ni tasa.
“Kadhalika, chembe za jeni zake zilichukuliwa na kuhifadhiwa jana kabla ya kifo chake kwa matumaini kwamba zitasaidia katika juhudi za siku za usoni za kuwazalisha faru kupitia teknolojia ya jeni na seli” Ol Pejeta wamesema.
Matumaini pekee sasa ya kuendeleza faru wa aina ya Northern White Rhino ni kupitia teknolojia ya kutungisha mbegu kwenye mayai ya mnyama nje ya mwili wa mnyama huyo, maarufu kama IVF.
Hilo linatarajiwa kufanyika kwa kutumia mayai yaliyovunwa kutoka kwa faru jike walio hai kwa sasa pamoja na mbegu za kiume kutoka kwa faru wengine wa Kaskazini.
Shughuli ya kutungisha mbegu mayai hayo ikifanikiwa, basi faru wa karibu aina ya Southern White Rhino watatumiwa kubeba mimba hiyo.
Mwaka uliopita, shirika la Ol Pejeta lilizindua kampeni ya kuchangisha fedha kupitia kufungua akaunti kwenye mtandao wa kutafuta wapenzi wa Tinder.
Lengo lilikuwa kuchangisha dola milioni 9 zitakazofadhili utafiti wa kutafuta mbinu mbadala za kutumia mbegu zao kuzalisha.
Tinder inaongoza ulimwenguni miongoni mwa mitandao ya kijamii inayotumika kutafuta marafiki na wapenzi.
Kupitia kampeni #TheMostEligibleBachelor, Tinder walitumai picha ya Sudan ingeonekana katika mataifa 190 ulimwenguni.
Kampeni hiyo ilidhaniwa kuwa njia pekee iliyosalia ya kuokoa faru hao wanaokabiliwa na hatari kubwa ya kuangamia.

No comments:

Post a Comment