Thursday, 15 March 2018

Femata yaomba serikali kuchunguza kimikali bandiaRais wa Femata, John Bina ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya kushughulikia kero za wachimbaji wadogo akizungumza nao wakati wa kikao cha kujadili soko la madini ya dhahabu kilichofanyika mkoani Geita. 

Joel Maduka, Geita

SERIKALI kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS),  imetakiwa kuchunguza kemikali bandia zinazouzwa na wafanyabiashara wasio waaminifu kwa wachimbaji wadogo wa madini hali inayowasababisha hasara.

Rais wa Shirikisho la wachimbaji wadogo wa madini nchini, (Femata) John Bina amesema hayo baada ya kikao kilichowakutanisha wachimbaji wadogo mkoani Geita ili kujadili namna Serikali itakavyoweza kuwajengea soko la madini kwa kanda ya ziwa.

Amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiuza kemikali bandia kwa wachimbaji wadogo na hivyo kuwasababishia hasara.

“Tunaomba serikali na TBS kuangalia dawa zinazoingia nchini ili kuhakikisha wanachunguza kemikali hizo kwani kwa sasa uzalishaji wa madini unashuka kwa kiasi kikubwa na nyie wachimbaji niwaombe muwe mnachunguza kabla ya kununua kwani kweli mnapata hasara kubwa,”amesisitiza Bina.

Mmoja wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu, Nuru Shabani amesema kuuziwa kemikali hizo bandia kumeanaathiri shughuli zake.

“Kiukweli tunaathirika sana na hili halina ubishi sasa hivi unaweza kununua tani moja ya kaboni unakuta inapitisha bila ya kushika mali ina maana hadi iwe na pipim kuanzia mia saba hadi mia nane, Ila kwa sasa nashukuru walau serikali imetambua mchango wetu na imetuthamini mimi nilikuwa naomba kupitia Kitengo chetu tuwe na wasimamizi ambao watatusaidia kubaini kemikali hizi,”amesema Nuru.

Bina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya kushughulikia kero za wachimbaji wadogo amesema pamoja na matatizo hayo lakini wachimbaji hao wamekubaliana kuanzishwa soko la madini mkoani Mwanza ili kudhibiti vitendo vya utoroshwaji wa madini.

No comments:

Post a Comment