Tuesday, 20 March 2018

Hakimu ataka sababu kwanini Nabii Tito haletwi mahakamani


Nabii Tito

Mary Meshack, Dodoma

HAKIMU Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Dodoma, James Kayaremaha, ametaka kupewa maelezo rasmi yanayoelezea kwa nini mshtakiwa Tito Machibya (Nabii Tito) hafikishwi mahakamani.

Kayaremaha alihoji hilo jana mahakamani hapo baada ya mshtakiwa huyo mkazi wa Ng'ong'ona Manispaa ya Dodoma, anayekabiliwa na kesi ya kutaka kujiua kwa kutumia wembe, kutofikishwa mahakamani kwa mara ya pili mfululizo na kusababisha kesi yake kuahirishwa. 

Hakimu huyo amesema, mshtakiwa huyo anapaswa kufikishwa mahakamani ili aendelee na kesi inayomkabili na siyo kuahirishwa kila wakati kwa kutofishwa mahakamani.

Hata hivyo, akizungumza mahakamani hapo jana, askari Magereza mmoja amedai kuwa, mshtakiwa huyo bado yupo Taasisi ya magonjwa ya akili ya Mirembe kwa ajili ya matibabu.

Askari huyo ambaye hakutaja jina lake amesema,  tangu mahakama ilipoamuru Nabii Tito afanyiwe vipimo vya kujua kama ana ugonjwa wa akili mwezi Februari mwaka huu, bado hajamaliza siku za uchunguzi wa vipimo hivyo, yupo Mirembe si kwenye gereza la mahabusi Isanga.

"Mheshimiwa, Tito bado yupo kwenye kitengo cha 'Blood more cha 'taasisi ya  Mirembe anaendelea na matibabu ya ugonjwa wa akili ,” amesema askari huyo 

Hata hivyo, Hakimu Karayemaha ameendelea kusisitiza kwamba mshtakiwa huyo shurti afikishwe mahakamani tarehe ilijayo ya kesi yake.

“Na kama kuna ulazima wa mshtakiwa kutofikishwa mahakamani, naomba nipate maelezo rasmi yanayokwamishwa kufikishwa mahakamani, “amesema Kayaremaha. Kesi hiyo imeahirishwa hadi April 5,  mwaka huu itakapotajwa tena.

No comments:

Post a Comment