Friday, 30 March 2018

Hakuna tishio la kiusalama nchini - Mambo ya NjeWaziri wa Mambo ya Nje na Ushirika wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga.


WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema hakuna tishio la usalama nchini kama inavyoenezwa katika mitandao ya kijamii kuwa April 26 mwaka huu kutakuwa na maandamano nchini na kuwataka wanadiplomasia, raia wa kigeni na wananchi kupuuza taarifa hizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imeeleza;

Kumekuwa na taarifa kwenye mitandao ya kijamii zinazosambazwa na watu wasioitakia mema nchi, zinazotishia usalama wa raia na mali zao. Taarifa hizo zimewatia hofu baadhi ya raia wa kigeni na wanadiplomasia wanaofanya kazi na kuishi hapa nchini.

Taarifa hizo zimekuwa zikidai kuwa kutakuwa na maandamano yatakayofanyika Aprili 26, 2018 zinaonya raia wa kigeni wasiende Zanzibar katika kipindi cha Sikukuu ya Pasaka na sherehe za Muungano kwa sababu za kiusalama.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawakikishia wanadiplomasia na raia wote wa kigeni wanaofanya kazi na kuishi nchini na wananchi kwa ujumla kuwa waendelee na shughuli zao ikiwemo kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine bila hofu yoyote kwa kuwa hakuna dalili zozote za uvunjivu wa amani, usalama na utulivu wa nchini.

Vyombo vya usalama vipo makini vinatekeleza majukumu yake ipasavyo kuhakikisha kuwa matukio yote ya uhalifu yanadhibitiwa kabla ya kuleta madhara kwa umma.

Hivyo, Wizara inawaomba wanadiplomasia, raia wa kigeni wanaoishi nchini na wananchi kwa ujumla kuzipuuza taarifa hizo. Wananchi waeendelee kushirikiana kwa ukaribu na serikali yao kupata taarifa sahihi kutoka vyanzo vinavyoaminika badala ya kutegemea propanganda za watu wanaotumia mitandao ya kijamii kwa maslahi binafsi.

No comments:

Post a Comment