Friday, 30 March 2018

Idadi ya watalii wanaoingia nchini 'yapaa'


Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma

TANZANIA imefanikiwa kuongeza idadi ya watalii kutoka 1,284,279 mwaka 2016 hadi 1,327,143  mwaka 2017. Ongezeko hilo ni dalili njema kwa mapato ya taifa.

Akizungumza wakati wa kikao cha baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Mali Asili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala amesema wizara hiyo itaendelea kuvutia watalii zaidi ili kukuza utalii na kuongeza pato la taifa.

“Mapato yanayotokana na utalii yameongezeka kutoka dola za Marekani Bilioni 2.1 mwaka 2016 hadi bilioni 2.2 mwaka 2017,” amesisitiza Kigwangala.
Akifafanua Dk. Kigwangala amesema lengo la Serikali ni kuona mafanikio haya yanazidi kuimarika, hivyo kila mtumishi katika wizara hiyo lazima atimize wajibu wake ipasavyo.

Ameongeza kuwa ili kufanikisha majukumu ya wizara hiyo ipasavyo ni muhimu kuwa na bajeti ambayo itawezesha kushughulikia changamoto za migogoro ya mipaka katika maeneo ya hifadhi, kufanya mapitio ya sera, Sheria na kanuni mbalimbali, upungufu wa watumishi, uhaba wa vitendea kazi, kutoa elimu ya maadili na kusimamia watumishi.

Kwa upande wake katibu mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudensi Milanzi amesema kuwa watazingatia ushauri unaotolewa na watumishi wake ili kuongeza tija katika kutatua changamoto zinazojitokeza.

“Wizara itaendelea kupambana dhidi ya ujangili, biashara haramu ya nyara na magogo na kuwachukulia hatua kali watumishi wote watakaogundulika kukiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kushiriki katika vitendo hivyo,” amesisitiza Meja Jenerali Milanzi.

No comments:

Post a Comment