Wednesday, 28 March 2018

JK kuongoza harambee Lindi sekondari


Rais mstaafu Jakaya Kikwete

Mwandishi Wetu, Lindi

RAIS msaatafu, Jakaya Kikwete leo anatarajiwa kuongoza harambee ya uchangiaji wa sh. bilioni 2.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Lindi iliyoungua moto mwaka 2016 na kusababisha hasara kubwa.

Mkuu wa mkoa huo, Godfrey Zambi amethibitisha hilo na kufafanua kuwa fedha hizo zinahitajika haraka ili kuirejesha shule hiyo katika hali yake ya awali.

Amesema fedha hizo pamoja na mambo mengine zitatumika kujenga majengo ya gharofa ili iwe na hadhi ya kitaifa kama ambavyo inapokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.

“Shule ya sekondari Lindi yenye kidato cha kwanza hadi cha sita iliungua moto usiku wa kuamkia Julai 10 mwaka 2016  ambapo madarasa tisa ikiwemo maabara na vitu vilivyomo, viti na meza zaidi ya 300  vikiwa na thamani ya sh. Bilioni 1 viliteketea,” amesema.

Zambi ameongeza kuwa katika kuhakikisha shule hiyo inajengwa wamefanya harambee na kukusanya zaidi ya sh. milioni 334 kati  ya milioni 444.

Amesema kati ya fedha hizo walifanikiwa kuanza ujenzi na kampuni ya Suma JKT kwa usimamizi wa wataalamu wa kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

“Harambee itafanyika mkoa wa Dar es Salaam, Machi 29 katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere ambapo mgeni rasmi atakuwa rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete naomba wana Lindi na wapenda maendeleo kujitokeza kwa wingi,” amesema.

Zambi ametoa namba za kuchangia fedha za ujenzi huo, kupitia Akaunti ya benki ya CRDB namba 0152208612700 jina la akaunti ni Lindi Education basket fund.

“Pia kwa wale ambao watatumia mtandao wa simu Mpesa namba 0768448410 jina Lindi regional admistrative  na 0685 72 1721 Lindi sekondari.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa amesema hajisikii vizuri mkoa huo kushika mkia na hivyo aliwataka maofisa elimu, wakuu wa shule kuhakikisha wanasimamia shule hiyo inafanya vizuri zaidi.

“Nimewaagiza wote hapa sitaki kusikia Lindi inakuwa nyuma kielimu, na hakuna ofisa hata mmoja anayekaa ndani bila kufanya kazi kila mmoja anatakiwa kuwa mkaguzi wa kuangalia maendeleo ya shule, mimi mwenyewe ni mkaguzi namba moja hivyo na wazazi pia wawasimamie watoto wao kufanikisha hilo,’’amesema.

Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi

No comments:

Post a Comment