Tuesday, 27 March 2018

Kalemani ahimiza wakandarasi kuunganisha umeme vijiji vitatu kwa wiki


Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani akizindua huduma ya umeme Rea awamu ya tatu kwenye kijii cha Magumbani, kata ya Moa, wilayani Mkinga. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Mkinga,Yona Mark na Mwenyekiti wa kitongoji cha Mbuluni Selemani Omari.

Mwandishi Wetu, Tanga
WAZIRI  wa Nishati Dk. Medard Kalemani amewaagiza Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), kuhakikisha wanaunganisha umeme kwenye vijiji vitatu kila wiki ili kutoa fursa kwa wananchi ya kufikiwa na huduma hiyo muhimu.

Dk. Kalemani ametoa kauli hiyo leo wakati akizindua upatikanaji wa huduma ya umeme chini ya mradi wa usambazaji wa Rea Awamu ya Tatu katika kijiji cha Magumbani, wilayani Mkinga, mkoa wa Tanga.

Uzinduzi huo umefanyika sanjari na uwashwaji  umeme katika kijiji hicho ili kuwawezesha kupata huduma hiyo ambayo haikuwepo awali katika eneo hilo.

Amesema uzinduzi huo ni matokeo ya jitihada za serikali za kuhakikisha inafikia malengo ya kuwapelekea umeme watanzania wote ifikapo mwaka 2021/2022 ili waweze kunufaika kupitia huduma hiyo.

“Leo tutaangalia mlipowasha lakini niwaagize wakandarasi tunataka kuona kila wiki vijiji vitatu vinawashwa umeme kwani wananchi wanauhitaji mkubwa wa kufikiwa na huduma hiyo hivyo hakikisheni hilo mnalitilia mkazo mkubwa,” amesema.

Hata hivyo amesema bado kuna changamoto ya wananchi kutapeliwa na mafundi ambao wamekuwa wakiwabambikia bei kuwaambia walipe kidogo kabla ya kulipia 27,000 ambazo wanazopaswa kulipa.

“Mameneja na wakandarasi tuna changamoto wananchi kunatapeliwa kuna tabia imezuka mafundi wanawabambikia bei wanaawaambia walipe kidogo kabla ya kulipa 27,000 labda niwaambie tu kwamba mtu wa namna hiyo atapobainika atachukuliwa hatua kali za kisheria,”amesema waziri huyo.

Amesema mradi huo utakwenda kila kijiji, kitongoji na nyumba kwa nyumba huku akieleza hata kama nyumba unayokaa utaona hakuna sehemu ya kutundukia waya weka hata kwenye mti ili mradi uweze kufikiwa na huduma hiyo.

Aidha, amesema kusudio jingine aliloendea huko ni kuweka msukumo kwa wakandarasi wafanye kazi usiku na mchana ili waweze kumaliza mradi huo kwa wakati.

Waziri huyo pia aliwataka wananchi kuendelea kutunza miundombinu ya umeme ikiwemo Transfoma kwa kuhakikisha haiibiwi yakiwemo mafuta ya transifoma. (Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha).

No comments:

Post a Comment