Thursday, 22 March 2018

Kamati ya Bunge yawasha umeme vijiji vitatu
Mwandishi Wetu

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imepewa heshima ya kuwasha umeme katika vijiji vitatu ambavyo huduma ya kupeleka umeme imekamilika.

Mchakato huo umefanyika kwa nyakati tofauti, Machi 15 hadi 18 Mwaka huu, wakati wa ziara ya Kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta za nishati na madini katika mikoa kadhaa nchini.

Vijiji vilivyowashiwa umeme ni Nyabange kilichopo wilaya ya Butiama mkoani Mara, kijiji cha Idala wilayani Nzega pamoja na Kisaki kilichopo mkoa wa Singida.

Akitoa ufafanuzi kwa kamati husika, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema vijiji hivyo vimepata huduma ya umeme kupitia mpango wa upelekaji umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) pamoja na mradi mkubwa wa umeme wa Backbone.

Mbali na kuwasha umeme katika vijiji hivyo vitatu, kamati pia ilitembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme katika vijiji vya Muryaza na Busegwe wilayani Butiama, vijiji vya Negezi, Mwaweya na Bulimba wilayani Kishapu, mkoa wa Shinyanga, Kitangiri wilayani Nzega pamoja na vijiji vya Kisaki na Nkunikana mkoa wa Singida.

Pia kamati ilikagua Kituo cha Kupooza Umeme cha Singida ambapo ujenzi wa mradi wa Singida, Arusha na Namanga utaanzia ikiwa ni pamoja na upanuzi wa kituo hicho unaoendelea kupitia Backbone.

Katika ziara hiyo, viongozi mbalimbali wa wizara walishiriki, akiwemo Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Kamishna wa Nishati Mhandisi Innocent Luoga pamoja na viongozi kutoka Rea na wengine kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

No comments:

Post a Comment