Wednesday, 14 March 2018

Katekista Mwita: Wakristo hawaandamani barabaraniClaudia Kayombo

SIKU chache zikiwa zimepita tangu Rais Dk. John Magufuli apige marufuku maandamano yanayodaiwa kupangwa kufanyika Aprili 26, mwaka huu, wakristo wamepewa mwito wa kuyapa kisogo.

Kateksta Fidelis Mwita wa Parokia ya Thomas Mtume Chanika, amesema wakristo wanapokutana na changamoto za aina yoyote zikiwemo za kisiasa wanamfikisha Mungu malalamiko yao kwa kufunga na kusali na si vinginevyo.

Ameyasema hayo Dominika iliyopita ambayo ni ya nne ya Kwarema wakati akihubiri katika Ibada ya Misa Takatifu, iliyoongozwa na paroko msaidizi wa parokia hiyo, Padri Jobi Joseph.

“Kama unasugua goti kuomba hupati, tafakari kwanza njia zako, Mungu ana upenda Ulimwengu ndiyo maana amemtuma mwanaye wa pekee aje kutukomboa kupitia mateso.

“Tunapojiita wakristo matendo yetu yafanane naye, watu wanaotuzunguka watutambue kuwa wakristo kupitia matendo yetu,” amesema.

Kuhusu chaguzi mbalimbali zinazofanyika kanisani, amesema viongozi wanakabiliwa na changamoto za kusemwa na waliowachagua ambao wanakiuka kanuni na taratibu za kanisa.

Amefafanua kuwa viongozi wa kanisani wanachaguliwa kwa kuongozwa na roho mtakatifu hivyo kama kuna mtu au kundi la watu anayewasema ana mkufuru roho huyo.

“Tujifunze kuwaheshimu wengine hasa tuliowapa dhamana ya uongozi. Kabla hatujawachagua tunamwomba Roho Mtakatifu atuongoze, tunapowaweka madarakani halafu kuwasema tunamdharau Roho Mtakati,” amesema Katekista Mwita.

Ametoa mwito kwa jamii kufanya toba na matendo mema hususan kwa wasiojiweza katika kipindi hiki cha Kwaresma, ambapo wakristo wa madhehebu mbalimbali duniani wakiwemo Wakatoliki wapo katika mfungo huo.

No comments:

Post a Comment