Thursday, 22 March 2018

Katibu wizara ya ujenzi awataka wafanyakazi kuchapa kazi


Mhandisi Joseph Nyamhanga


Mwandishi Wetu, Dodoma

KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga amewataka wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo na watumishi wote kutimiza wajibu wao kwa kutumia muda wao wa kazi kufanya kazi kwa bidii.

Ameyasema hayo wakati akizindua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekta ya Uchukuzi leo mkoani Dodoma.

Mhandisi Nyamhanga amesema wizara hiyo inatambua mchango mkubwa wa wafanyakazi wa ngazi zote katika kufanikisha shughuli za sekta hiyo hali inayochochea sekta ya uchukuzi na utabiri wa hali ya hewa kutoa huduma zenye ubora wa hali ya juu ndani na nje ya nchi.

Akifafanua Mhandisi Nyamhanga amesema sekta za uchukuzi na tabiri za hali ya hewa zina jukumu la kutoa huduma zenye ubora wa kiwango cha juu ndani na nje ya nchi.

“Dhana hii ya ushirikishwaji wa wafanyakazi ni muhimu kwa jumuia yoyote na katika ngazi yeyote, hivyo niwashukuru sana kwa kuzingatia dhana hii muhimu na ninashauri muiendeleze,” amesisitiza Nyamhanga.

Amewataka wajumbe wa baraza hilo kuzingatia maelekezo ya kisheria wakati wa kuchangia taarifa muhimu za sekta na kushirikiana katika utekelezaji wake ili kufikia malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi na kusisitiza kuwa haitosita kumwajibisha mtumishi yeyote ambaye ataonekana kuwa chanzo cha kutotimiza malengo ya bajeti na mpango kazi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi la Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi), Dk.Leonard Chamuriho amesema wafanyakazi wa sekta ya uchukuzi kama walivyo watumishi wengine katika utumishi wa umma wamejipanga kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi, uadilifu, juhudi na maarifa katika kutimiza wajibu wao ili kuchangia katika kutekeleza malengo ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo.

“Tunafahamu wazi kwamba kutokusimamiwa na kuendelezwa kwa miundombinu ya uchukuzi na huduma zake hakutowezesha sekta nyingine za kiuchumi na kijamii kukua na kuchangia katika maendeleo ya taifa,hivyo tutaendelea kuboresha miundombinu ya uchukuzi na huduma zake,”ameongeza Dk.Chamuriho.

No comments:

Post a Comment