Thursday, 8 March 2018

Kenya yakumbwa na upungufu mkubwa wa fedha


Waziri wa Fedha wa Kenya, Henry Rotich.
WIZARA ya Fedha nchini Kenya imekiri kuwa serikali imekumbwa na changamoto kubwa za kifedha na haiwezi kabisa kutimiza mahitaji yake.
Ufadhili wa miradi muhimu ya serikali umeathiriwa zikiwemo serikali za kaunti ambazo bajeti zao serikali itazipunguza kwa sh. bilioni 15 na 17 au dola 147,913,193 na 167,634,953.
Kutokana na ukosefu huo wa fedha, mashirika ya serikali yametakiwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kutumia fedha zilizopo kwa njia inayostahili.
"Kila shirika ni lazima lijizatiti. Tumebuni njia ya kupunguza matumizi. Tunapunguza matumizi kwa kila sekta ili kwenda sanjari na fedha zetu," amesema waziri wa fedha wa nchi hiyo Henry Rotich.
Ameongeza kuwa hali hiyo imetokana na kushindwa kutimiza malengo yake ya kukusanya ushuru baada ya kipindi kirefu cha shughuli za uchaguzi.
“Tumeongea na KRA jinsi tunaweza kukabiliana na hilo kupitia ukusanyaji wa kodi ya ndani na ya nje," Rotich aliiambia kamati ya seneti.
Kulingana na Rotich serikali inakabiliwa na upungufu wa ukusanyaji ushuru wa sh. bilioni 70 kwenye makadirio ya serikali ya mwaka 2017/2018.
Kutokana na hilo, kuna uwezekano kuwa wakenya watakumbwa na nyakati ngumu kwa sababu serikali itaendelea kukopa ndani ikishindana na watu, hali ambayo itachangia biashara ndogo kuwa na ugumu wa kupata mikopo kutoka benki.
Hadi Desemba mwaka uliopita, deni la Kenya lilikuwa sh. trilioni 4.55, ambalo limesababisha nchi kutenga asilimia 54 ya pato lake kulipa madeni.
Maseneta walitaka kujua ni kwa nini serikali za kaunti hazijapokea fedha kwa miezi minne licha ya seneti kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo.
Alijibu na kusema kuwa ni sh. bilioni 134 tu zimetolewa kwa serikali za kaunti kinyume na fedha zilizokuwa zikihitajika dola bilioni 302.

No comments:

Post a Comment