Rais Uhuru Kenyatta (kushoto) na Raila Odinga
RAIS wa Kenya Uhuru Kenyatta amekutana
na kiongozi wa muungano wa upinzani nchini humo, Raila Odinga katika ofisi yake
Jumba la Harambee, Nairobi.
Viongozi hao wamekubaliana kuundwe mpango wa pamoja wa kuangazia
utekelezaji wa malengo ya pamoja ya viongozi hao wawili, ambao utazinduliwa
rasmi karibuni.
Balozi Martin Kimani ataongoza kuundwa kwa mpango huo upande wa Rais
Kenyatta naye mshauri wa Odinga Paul Mwangi atamwakilisha Odinga, kwa mujibu wa
taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na Kenyatta na Odinga baada ya mkutano huo.
Mkutano huo umefanyika muda mfupi kabla ya Waziri wa Mambo ya
Nje wa Marekani, Rex Tillerson kuwasili nchini humo kwa ziara ya siku nne.
Marekani imekuwa ikihimiza kufanyika kwa mazungumzo na
mashauriano kutatua mzozo wa kisiasa uliolikumba taifa hilo baada ya uchaguzi
uliojaa utata mwaka jana.
Odinga alitangulia
kuhutubia taifa moja kwa moja na baadaye Kenyatta akatoa hotuba yake.
Kenyatta amesema wamekubaliana na Odinga kwamba taifa la Kenya
ni muhimu kuliko mtu binafsi na kwamba lazima viongozi washirikiane.
Rais huyo amesema siku za usoni za Kenya haziwezi kuongozwa na
uchaguzi ujao bali "uthabiti wa taifa."
"Demokrasia si mwisho wa kila kitu. Ni shughuli na nia ya
wananchi lazima iongoze."
"Tumekubaliana tutaleta pamoja wananchi na kujadiliana
kuhusu matatizo yanayoathiri taifa letu na wananchi, na kuunda taifa lenye
umoja na lililo imara ambapo hakuna raia anayehisi ametengwa."Huu ni
mwanzo mpya kwa taifa letu."Tunaweza kutofautiana lakini kusalia tukiwa
tumeungana kama Wakenya.
Odinga amesema kwa muda mrefu Kenya imeangazia kubadilisha
taasisi na miaka saba iliyopita katiba mpya ilianza kutekelezwa.
"Sasa lazima tuwe na ujasiri wa kukubali kwamba hilo
halijafanikiwa. Bado hatujabadilisha mengine," amesema Odinga.
"Ndugu yangu na mimi tumekutana pamoja leo na kusema
yamefikia kikomo. Tumekataa kuwa watu ambao chini yake Kenya imekuwa taifa
lililofeli."
Odinga mesema wamekubaliana kufanikisha mabadiliko
yatakayofanikiwa mageuzi nchini humo na pia kukomesha kulaumiana. Amewataka
Wakenya waunge mkono mpango wa viongozi hao wawili.
"Tumesafiri mbali sana kiasi kwamba hatuwezi kurudi tena
bandarini. Isitoshe, hatuwezi kufika tunakokwenda bila kufanya mabadiliko la
sivyo tutazama baharini," amesema Odinga.
"Tumekuja pamoja na ndugu yangu Kenyatta, tumeongea kwa
kirefu na kukubaliana kwamba tunataka kuunganisha Kenya iwe taifa moja.
Mgawanyiko ambao umekuwepo tangu uhuru utakwisha hapa na sisi. Tutembee
pamoja," amesema Odinga.
No comments:
Post a Comment