Friday, 16 March 2018

Kinyondo: Asilimia 10 ya Bajeti iguse kilimoSuleman Kasei

SERIKALI imeshauriwa kutenga asilimia 10 ya bajeti yake katika sekta ya kilimo ili kuchochea ukuaji wa uchumi na viwanda nchini.

Ushauri huo unakuja ikiwa ni siku chache baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kuwasilisha mapendekezo ya makusanyo na matumizi ya Bajeti ya mwaka 2018/19 ya sh. trilioni 32.4 huku kipaumbele kikubwa katika mwaka huo kikiwa ujenzi wa reli ya kisasa, ununuzi wa ndege, kuinua Shirika la Simu Tanzania (TTCL), uzalisahaji umeme eneo la Bonde la Mto Rufiji (Stigler Gourge).

Katika mapendekezo yalitowasilishwa na Waziri Mpango ya sh. trilioni 20 sawa na asilimia 63 zimetengwa kwa shughuli za kawaida na sh. trilioni 12 sawa na asilimia 37 zikitengwa kwa ajili ya maendeleo.

Ushauri huo umetolewa na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU), Dk. Godbether Kinyondo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam.

Dk. Kinyondo amesema sekta ya kilimo ni mtambuka ambayo ikipewa kipaumbele itaweza kugusa sekta mbalimbali, kama uchumi, miundombinu, elimu na afya.

Amesema kwa mujibu wa azimio la Maputo serikali zinapaswa kutenga asilimia 10 ya bajeti yake kwa ajili ya sekta ya kilimo hivyo ni lazima Serikali itekeleze azimio hilo kwa maslahi ya nchi na wananchi.

Mhadhiri huyo ambaye ni mchumi kitaalam amesema bajeti hiyo ingepaswa kujikita katika sekta ya kilimo na maji ambazo zinaajiri kundi kubwa la Watanzania hali ambayo itaonesha matokeo chanya kwa haraka.

Amesema iwapo kutakuwepo na uwekezaji mkubwa katika sekta hizo ni dhahiri sekta ya miundombinu, mawasiliano na anga zitapiga hatua pia.

“Huwezi kujikita katika kutengeneza reli ya mwendo kasi, viwanja vya ndege, ununuzi wa ndege na umeme huku ukiwa umeacha sekta ya kilimo inayoajiri kundi kubwa naamini kilimo kikipewa kipaumbele kitatoa matokeo chanya haraka,” amesema.

Amesema sekta ya kilimo inahitaji msukumo na uwekezaji mkubwa ili kuinua uchumi wa nchi na wananchi hasa wale wanaoishi jirani na njia ya reli.


Aidha, Dk. Kinyondo ameongeza kuwa sekta ya maji inapaswa kuangaliwa kwa jicho la kipekee kutokana na ukweli kuwa inachochea kilimo cha umwagiliaji.

Dk. Kinyondo amesema iwapo kilimo kitaweza kuchochea na kuongeza thamani ya bidhaa za ndani tofauti na ilivyo sasa ambapo asilimia kubwa ya bidhaa zinazotumika zinatoka nje.

Mhadhiri huyo amesema sekta hizo zikipata msukumo mkubwa kundi kubwa ambalo linapambana na kulea familia hasa la kina mama litapiga hatua za kuchumi.

No comments:

Post a Comment