Saturday, 31 March 2018

Kiwanda chafungwa kwa kukosa masokoMkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alipofanya ziara yake ya siku moja kutembelea viwanda vinane mjini Kibaha.

Julie Julian, Kibaha

SERIKALI imebaini kufungwa kiwanda cha kutengeneza nguzo za zege cha Hunnan Power cha mjini Kibaha, mkoani Pwani, baada ya kukosa tenda na soko.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, amebainika hilo wakati wa ziara yake ya kutembelea viwanda vinane vilivyoanza uzalishaji na ambavyo vipo kwenye hatua za ujenzi mjini hapa.

Kutokana na hali hiyo, kiwanda hicho kimebaki gofu na kupunguza ajira kutoka wafanyakazi 30 hadi wawili kwasasa tangu uzalishaji uanze mwezi Septemba mwaka jana.

Mhandisi Ndikilo amesema mkoa huo unadhamira ya kuwa ukanda wa viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali lakini endapo soko halikuwepo wawekezaji watakata tamaa.

Amesema mkoa una viwanda vinavyotengeneza nguzo za zege viwili ikiwemo Hunnan Power /Kibaha na East Africa infrastructure engineering Ltd kilichopo Fukayosi /Bagamoyo ambavyo vinahofiwa kushindwa kuendelea kuzalisha kwasababu ya bidhaa zake kukosa wateja.

“Katika ziara hii tumebaini changamoto ya kiwanda cha Hunnan Power  kukosa masoko na tenda huko shirika la umeme (Tanesco ), hawajapata tenda mara tatu.

“Hali hiyo imesababisha kiwanda hicho kufungwa, hakizalishi, mashine zimefungiwa ndani, kiwanda kimezungukwa nyasi, kimekuwa gofu na ajira hakuna” suala hili linaangusha juhudi za rais John Magufuli, mkoa na serikali,”amesema mhandisi Ndikilo.

Ndikilo amefafanua kuwa wawekezaji wanajitoa kuunga mkono na kuitikia mwito wa serikali wa kujenga viwanda lakini baadhi vinakumbana na changamoto ya ukosefu wa soko la uhakika.

Aliahidi kuzungumza na waziri mwenye dhamana na mkoa utafuatilia ili waziri wa nishati aweze kusaidia suala hilo.

Mkuu huyo wa mkoa aliitakaTanesco kuangalia kwa jicho la tatu tatizo hilo kwa kuangalia namna ya kutoa tenda ili kuinua viwanda hivyo. Alitaja changamoto nyingine alizofikishiwa kwenye ziara hiyo, kuwa ni umeme, maji barabara na vibali kutoka TFDA.

Amewasihi viongozi wa wilaya na halmashauri kuandika barua moja kwa moja kwa taasisi husika watatue matatizo hayo ili kuwavutia wawekezaji.

Awali akitoa taarifa ya kiwanda cha Hunnan Power, mkalimani wa kiwandani hapo, Suleiman Ramadhani alisema kilianza ujenzi Januari 2017 na kuanza uzalishaji Septemba mwaka huo huku kikigharimu dola milioni 2 na hakijawahi kuuza hata nguzo moja.

Amesema kiwanda hakifanyi kazi tangu Jananuari mwaka huu kwakuwa kinategemea tenda na soko.

Suleiman ameelezea kuwa wenye viwanda wanahitaji kujenga kiwanda kingine katika eneo hilo lakini wanashindwa kwasasa hadi hapo watakapopata wateja.

Mhandisi wa udhibiti wa mapato Tanesco mkoani Pwani, Fabian Rukiko amesema hawajawahi kutumia nguzo za zege mkoani hapo hadi hapo itakapohitajika.

Alikishauri kiwanda hicho kujitangaza kupitia kitengo cha mauzo na masoko kwani itasaidia kufanya ufuatiliaji na kushirikiana na wadau wakubwa watakaoweza kununua bidhaa hiyo muhimu ambayo inadumu kwa kipindi kirefu.

Novemba mwaka jana, waziri wa Nishati Dk. Merdard Kalemani alitembelea kiwanda cha nguzo za zege kilichopo Fukayosi na alilitaka shirika la umeme Tanesco kutumia nguzo zinazozalishwa nchini kwenye ujenzi wa miradi mikubwa.

No comments:

Post a Comment