Tuesday, 27 March 2018

Kuweni na upendo, umoja kama Utatu Mtakatifu - Nzigilwa


Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa

Claudia Kayombo, Dar es Salaam

MAPADRI  wa Kanisa Katoliki wameaswa kuwa na upendo na umoja katika kutekeleza majukumu yao kwa mfano wa Utatu Mtakatifu. Pia wajitoe kutoa huduma za kiroho na kimwili kwa waamini wao.

Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigilwa ametoa kauli hiyo leo wakati akihubiri katika ibada ya Sikukuu ya mapadri kwenye Kanisa Kuu la Kiaskofu la Mtakatifu Yosefu, jimboni hapa.

Katika ibada hiyo mapadri walikuwa wanarudia ahadi zao za upadri, lakini pia kulifanyika tukio la kubariki mafuta ya manukato, mafuta ya wakatekumeni, mafuta ya wagonjwa na kuwekwa wakfu mafuta ya Krisma takatifu.

“Katika kutimiza mapenzi ya Mungu tunatakiwa kujitoa sadaka, tuwe na upendo kama Kristo, umoja kama wa utatu mtakatifu, tukifanya hivyo tutakuwa tumefanya mapenzi ya Mungu.

"Ili tuweze kufanya utume wetu wa kipadri vizuri inatupasa kuzingatia alichosema Yesu kuwa tumtumikie Mungu peke yake, Yesu alisema hamwezi kumtumikia Mungu na mali, tamaa ya ulimwengu na anasa zake ni kutumikia miungu.

"Changamoto ya kanisa la sasa mapadri tunachukuliwa mno na ulimwengu hata walimwengu wenyewe wanatushangaa. Tuachane na malimwengu,tumtumikie Mungu peke yake.

“Tumtumikie Mungu popote na daima, nje ya hapo hatufanyi mapenzi Mungu.Tumtumikie Mungu kabisa na kikamilifu, tujitoe kabisa kwa Mungu, amesisitiza.

Amesema wapo miongoni mwa madri ambao wanaishi katika mahangaiko ya kutafuta raha za dunia matokeo yake wanakosa furaha ya kweli. 

“Angalia wenzetu mama Teresa wa Kalkuta na Papa Yohane Paulo wa pili waliishi kwa amani wakizingatia yale waliyoitiwa na Mungu yaani kumpenda na kumtumikia hata maisha yao tunayapigia mfano sasa. Mapadri tujitoe wazima wazima,” ameongeza.

Hata hivyo, Mhashamu Nzigilwa amesema amefurahi tangu mwaka huu uanze hajaletewa kesi inayohusu mapadri wa jimbo hilo kugombana, hali ambayo inaonesha wanajitahidi kuishi kwa upendo.

Misa takatifu ya kwanza aliiadhimisha Yesu Kristo mwenyewe Siku ya Alhamis Kuu katika kile chumba alipokula karamu ya mwisho na wanafunzi wake.

Askofu Mkuu wa jimbo hilo, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo aliongoza viapo hivyo vya mapadri, naye akiwaomba wamwombee aweze kutimiza majukumu yake ipasavyo.

No comments:

Post a Comment