Friday, 16 March 2018

Lissu afanyiwa upasuaji wa 19


Tundu Lissu

MBUNGE wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amewekewa chuma katika mguu wake wa kulia ili kuimarisha mfupa wa paja.

Rais huyo wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) alifanyiwa upasuaji huo juzi Machi 14, kama alivyoshauriwa na madaktari wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg nchini Ubelgiji.

Lissu amesema operesheni hiyo iliyochukua saa mbili, ilifanywa na timu ya madaktari bingwa chini ya uongozi wa Profesa Willem-Jan Mertsemakers.

“Operesheni ilienda vizuri na kwa sasa naendelea na dawa na mapumziko hospitalini kwa muda wa angalau wiki tatu zinazokuja.

“Wameniwekea chuma cha kuimarisha mfupa wote wa paja la kulia. Pia wamechukua vipimo ili kuangalia kama hakuna tatizo la bakteria kabla hawajafunga kabisa sehemu ya kwenye goti ambayo haijaunga hadi sasa,”amesema Lissu.

Mke wa Lissu, Alicia amesema anamshukuru Mungu kwamba upasuaji huo umekwenda vema. Huu ni upasuaji 19 tangu alipoanza kupatiwa matibabu Septemba mwaka jana baada ya kupigwa risasi akiwa mkoani Dodoma alikokuwa anahudhuria vikao vya Bunge.

No comments:

Post a Comment