Wednesday, 14 March 2018

Mabadiliko sera za misaada kikwazo kwa bajeti


Dk. Philip Mpango

Mary Meshack,Dodoma

MABADILIKO ya sera za misaada katika nchi zilizokuwa zikiipatia Tanzania misaada ya kibajeti ni miongoni mwa changamoto za utekelezaji wa mpango  wa bajeti kwa mwaka 2017/18 .

Changamoto nyingine katika kipindi hicho ni nwamko mdogo wa kulipa kodi hususan kuzingatia matumizi ya mashine za kielektroniki na masharti magumu ya upatikanaji wamikopo ya kibiashara kutoka nje.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango amesema hayo mjini hapa na kwamba changamoto hizo zilisababisha kutofikiwa kwa malengo ya makusanyo ya mapato katika mpango wa bajeti katika kipindi hicho.

Pia amesema utekelezaji wa mpango huo uliathiriwa na uwepo wa malimbikizo ya madai, ugumu wa upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji, matayarisho hafifu ya miradi na mabadiliko ya tabianchi ambayo yalisababisha uharibifu wa miundombinu ya usafiri kutokana na mvua  kubwa katika baadhi ya maeneo.

Hata hivyo, Dk. Mpango  amesema hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu na faida za kulipa kodi kwa kutumia mitandao ya kielektroniki, kuwezesha mifumo ya kodi kutambua malipo kwa kutumia huduma za simu za mkononi na kukusanya kodi mbalimbali.

Pia kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa stempu za kodi kwenye viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa na  zile zinazoingizwa nchini huku akisema mfumo huo utasaidia kupata taarifa kamili  za uzalishaji viwandani pale tu kiwanda kinapofanya uzalishaji na kupunguza uvujaji wa mapato ya serikali.


No comments:

Post a Comment