Friday, 23 March 2018

Mahakama yatoa hukumu kesi ya Nguza Viking, mwanawe


Nguza Viking (kulia), na mwanawe Johnson Nguza siku waliyokuwa wanatoka gerezani baada ya msamaha wa rais
MAHAKAMA ya Afrika na Haki za Binadamu (AfCHPR) inatoa hukumu katika kesi iliyowasilishwa na wanamuziki Nguza Viking maarufu Babu Seya na mwanaye, Johnson Nguza 'Papii Kocha' dhidi ya serikali ya Tanzania katika mahakama hiyo.
Wawili hao waliwasilisha rufaa katika mahakama hiyo mwaka 2015 kupinga hukumu ya kifungo cha maisha iliyokuwa imetolewa dhidi yao.
Walikuwa wanatumikia kifungo cha maisha jela kwa kuwabaka wasichana 10 wa shule waliokuwa na umri wa kati ya miaka 6 na 8 mwaka 2003. Walikuwa wametumikia kifungo cha miaka 13 kufikia wakati wa kupewa msamaha
Babu Seya ambaye ni miongoni mwa wafungwa 1,821 waliosamehewa na Rais John Magufuli siku ya Uhuru wa Tanganyika mnamo 9 Desemba, 2017. Wengine 8157 walipunguziwa adhabu zao.
Wawili hao ndio walioimba kibao maarufu cha 'Seya' na walikuwa kati ya wafungwa 61 waliokuwa wamehukumiwa kufungwa maisha au kunyongwa ambao walinufaika kutokana na msamaha wa rais.
Hukumu katika kesi yao ilikuwa imepangiwa kusomwa Jumatano wiki hii lakini baadaye ikaahirishwa hadi leo.
Mahakama hiyo kupitia ujumbe Facebook imesema hukumu imeanza kusomwa mwendo wa saa tano saa za Afrika Mashariki. Hatua ya Dk. Magufuli kuwasamehea wawili hao ilishutumiwa na watetezi wa haki za watoto na wanawake.
Kate McAlpine, mkurugenzi wa shirika la Community for Children Rights lenye makao yake Arusha aliiambia BBC wakati huo kwamba alikuwa "ameshtushwa lakini hakushangazwa" na hatua ya rais huyo. Alisema hatua hiyo ilionesha 'uelewa mdogo' wa kiongozi huyo kuhusu masuala ya udhalilishaji wa watoto.
Alilinganisha hatua hiyo na tamko la Rais Magufuli kwamba wasichana wanaoshika mimba hawafai kuwa shuleni.
“Huwa hafahamu vema mambo, hasa yanayohusu watoto kama waathiriwa. Wasichana wanaokwenda shule hushika mimba kwa sababu mara nyingi ni waathiriwa wa udhalilishaji,” alisema McAlpine.
Kwa kuwa wawili hao walishasamehewa na rais, uwezekano wao kuchukuliwa hatua iwapo hukumu ya kifungo dhidi yao itadumishwa ni mdogo sana.
Hata hivyo, iwapo watapatikana bila hatia, kuna uwezekano huenda wakawasilisha kesi wakitaka walipwe fidia kwa kipindi ambacho walikaa gerezani.
Nguza Viking na Johnson Nguza ni baba na mwanaye na ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao walikuwa wanamuziki Dar es Salaam.
Wote walikamatwa Oktoba 12, 2003 na kuzuiliwa kituo cha polisi cha Magomeni ambapo baadaye walifikishwa kizimbani mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Oktoba 16, 2003 na kufunguliwa mashtaka 10 ya ubakaji na 11 ya ulawiti.
Waathiriwa wao walikuwa watoto wa kati ya miaka sita na nane, na walikuwa wote kutoka darasa moja.Waathiriwa hao walidaiwa kubakwa na kulawitiwa kwa zamu na wanaume watano.
Mnamo 25 Juni, 2004 hakimu aliwapata na hatia na kuwafunga jela Nguza na wanawe watatu. Mshtakiwa wa nne, ambaye alikuwa mwalimu, hakupatikana na hatia. Washtakiwa walikata rufaa Mahakama Kuu lakini ikatupwa.Walikata rufaa tena katika Mahakama ya Rufaa.
Wawili kupatikana bila hatia
Mwaka 2010 rufaa yao ilisikilizwa na Oktoba 30 Majaji Nathalia Kimaro, akisaidiana na Mbarouk Mbarouk na Salum Masati katika Mahakama ya Rufaa wakawaachilia huru Nguza Mashine na Francis Nguza baada ya kuwapata bila hatia.
Babu Seya na mwanaye Papii Kocha walipatikana na hatia na hivyo kuendelea kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela. Majaji walisema kuna uthibitisho kuwa warufani hao wawili waliwabaka watoto wa shule ya msingi mwaka 2003.
Kesi hiyo iliwashtua mashabiki wa mwanamuziki Viking nchini Tanzania na kanda nzima ya Afrika Mashariki. Mwanamuziki huyo mwenye kuimba nyimbo za rhumba, ambaye ni mzaliwa wa DRC, ameishi hapa nchini kwa muda wa miaka mingi na kuwa na mashabiki wengi.

No comments:

Post a Comment