Wednesday, 21 March 2018

Majaliwa aguswa na jitihada za mama mlemavu amsaidia milioni 5/-


Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemkabidhi Tecla Hamidu ambaye ni mlemavu wa miguu sh. milioni tano ili aongeze mtaji wake.

Ametoa fedha hizo jana (Jumanne, Machi 20, 2018) ikiwa ni katika kutimiza ahadi yake aliyoitoa Februari 22, mwaka huu 2018 kwenye Mkutano wa Sita wa Wamiliki wa Viwanda na Watumiaji wa simbomilia (barcodes).

Waziri Mkuu alitoa ahadi hiyo baada ya Bibi Tecla ambaye ni mjasiriamali anayejihusisha na ushonaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo nguo kumuomba amchangie sh. 500,000 ili aweze kuongezea mtaji wake.

Wakati akimkabidhi fedha hizo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema anatarajia zitamsaidia kuongeza  mtaji wake, hivyo atazalisha bidhaa nyingi zenye ubora unaohitajika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Bibi Tecla alimshukuru Waziri Mkuu kwa msaada huo na ameahidi kuzitumia fedha hizo kama ilivyo kusudiwa.

“Nashukuru kwa msaada huu kwani kuna watu wanakopa sh. laki mbili ili waongeze mitaji, lakini mimi leo nimepewa milioni tano bure na kiongozi wetu,”

Amesema licha ya kukabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa masoko ana amini tatizo hilo litakuwa historia baada ya kuwa na mtaji wa kutosha kwa kuwa atakwenda kuzalisha bidhaa zenye ubora zaidi.

No comments:

Post a Comment