Saturday, 24 March 2018

Makinda afichua siri ya ushindi wa wanawakeMama Anne Makinda 

SPIKA mstaafu wa Bunge, Mama Anne Makinda ametoa elimu ya uongozi wa Kijinsia kwa madiwani wanawake wa mkoa wa Dar es Salaam katika warsha ya siku moja iliyoandaliwa na TGNP Mtandao ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo.

Akizungumza katika warsha hiyo, Makinda amesema suala la kuwajengea uwezo wanawake linapaswa kuanza mapema mara tu baada ya kumalizika uchaguzi ili kupata muda zaidi wa viongozi hao kupata elimu stahiki, kwani mara nyingi elimu hiyo hucheleweshwa kutolewa.

Kimsingi muda huu tumechelewa mikakati ya kuanza kumuwezesha kiongozi mwanamke hupaswa kuanza mara baada ya kumalizika uchaguzi, hii itatusaidia hata kujipanga mapema uongozini…,” amesema Mama Makinda.

Amewataka wanawake wote viongozi kuwa pamoja hasa wanapopigania masuala yao kwani umoja mara zote ni nguvu na utengano ni udhaifu. 

Changamoto za wanawake hazitofautiani kiitikadi za chama, rangi wala imani hivyo kuna kila sababu ya kuungana pale wanapogombea ajenda za wanawake.

Pamoja na hayo amewataka madiwani wanawake kujipanga kimikakati na kutokubali kuondolewa katika nafasi za uongozi kizembe, kwani uwezo wa kuwatumikia wananchi wanao tena wa kiwango kikubwa kama watajipanga vizuri.

“…Hivi unakubalije mtu aliye nje kuja kukutoa katika nafasi yako kirahisi rahisi ilhali wewe upo karibu na wananchi, usikubali tuwaoneshe kwa vitendo tulioingia tusitoke kirahisi bila kupenda labda tupande ngazi lakini sio kushuka,” amesisitiza.

Aidha, amewaomba kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wa kiume kwani idadi yao ni kubwa hivyo ushawishi pekee ndio unaweza kuongezea nguvu ajenda zao.

Amebainisha idadi ya madiwani na wabunge wa kiume ni kubwa ikilinganishwa na wao hivyo njia pekee ya wao kufanikiwa ni kujenga urafiki, ukaribu na ushawishi kwa agenda anuai zinazobebwa na wanawake.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Wanawake Tanzania (TWPG), Suzan Lyimo akizungumza na madiwani hao amewataka kuwa kitu kimoja hasa wanapopigania masuala ya msingi ya kumuwezesha mwanamke.

Amesema kama wanawake hawatakuwa kitu kimoja hawawezi kufanikiwa katika agenda zao. Hata hivyo, ameongeza kuwa usawa wa kijinsia unapaswa kuanzia ndani ya vyama vya siasa kwani ndipo mipango mingi ya chama hupangwa kwa utekelezaji zaidi.

No comments:

Post a Comment