Wednesday, 21 March 2018

Mama Samia amtaka IGP kutowaonea haya Polisi wanaokiuka maadili


Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akipeana mikono na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba za polisi 36 Mfikiwa Chake Chake Pemba. Kulia kwa IGP ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni.


Peter Simon

MAKAMU wa Rais Mama Samia Suluhu  Hassan amemtaka Mkuu wa  Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro kuwachukulia hatua mara moja askari polisi ambao wamekiuka maadili na taratibu za jeshi hilo katika mkoa wa Kusini Pemba.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa kuwekwa jiwe la msingi ujenzi wa nyumba 36 za askari polisi katika eneo la Mfikiwe, wilaya ya Chake Chake, mkoa wa Kusini Pemba.

Makamu wa Rais ametoa pongezi kwa Jeshi la Polisi nchini kwa kuhakikisha nchi inakuwa tulivu na yenye amani pia ametoa pongezi kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kwa kusimamia vema mchakato wa ujenzi wa nyumba za Polisi.

Makamu wa Rais pia ametoa pongezi nyingine kwa kampuni ya Twiga Cement kwa kutoa Saruji mifuko zaidi ya elfu sita pamoja na kampuni za Shubash Patel kwa kuchangia vifaa vingine vya ujenzi.

Awali Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni alipongeza Jeshi la Polisi kwa kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya na kusema yeyote atakayevunja sheria achukuliwe hatua bila kujali wadhifa au umaarufu wake.

Kwa Upende wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini ameahidi kufanya kazi kwa taratibu na sheria lakini pia amewaasa wanasiasa wanaochochea vurugu kwani nao watachukuliwa hatua za kisheria kama wahalifu na si wanasiasa.

Ziara ya Makamu wa Rais imekamilika jana ambapo pia alitembelea Hospitali ya Abdalah Mzee ambapo alijionea vifaa vya kisasa vilivyowekwa na huduma bora zinazotolewa.

Makamu wa Rais pia ameweka mawe ya Msingi katika ujenzi wa madarasa kwenye skuli (shuele) ya sekondari ya Ali Khamis Camp pamoja na ujenzi wa Tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ole.

No comments:

Post a Comment