Saturday, 24 March 2018

Mama Samia, Rodger wajadili kuwakwamua wanawake nchiniMakamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan (kulia) akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Bill na Melinda Gates, Rodger Voorhies kwenye makazi yake, Kilimani mjini Dodoma. (PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)

Mwandishi Wetu, Dodoma


MAKAMU wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan jana (Machi 23, 2018) amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Bill & Melinda Gates Foundation, Rodger Voorhies kwenye makazi yake, Kilimani mjini Dodoma.

Makamu wa Rais amesema amezungumza mambo mengi na Rodger hasa kwenye masuala ya afya, uwezeshaji wanawake kiuchumi, kuwatoa kwenye kilimo cha sasa na kuwaingiza kwenye kile cha biashara lakini pia kuongeza thamani ya mazao na mambo ya masoko.

Makamu wa Rais amesema wamezungumza namna ya kuwarasimisha wanawake wa vijijini na wanawake wakulima ikiwa pamoja na uwezekano wa wale wa vijijini kupata mikopo.

Aidha, Mama Samia alizungumzia suala la upatikanaji wa maji safi na salama hasa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam ambapo mara kwa mara kumekuwa na mlipuko ya magojwa ya kipindu pindu.

Kwa upande wake Rodger Voorhies amesema wamekuja kwa Makamu wa Rais kuzungumza kuhusu shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo hapa nchini hasa katika masuala ya kilimo na afya na mkakati mpya wa kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Aidha, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua kubwa ambayo imepiga katika kuwajumuisha wanawake kwenye masuala yanayohusu fedha. Mkurugenzi huyo ameahidi ushirikiano mkubwa kwa Serikali ya Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya taasisi hiyo.

No comments:

Post a Comment