Tuesday, 6 March 2018

Manispaa Ilala yapitisha bajeti yake


Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko
Suleiman Kasei
HALMASHAURI ya manispaa ya Ilala imepitisha bajeti ya sh. billioni 287 kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Imepitishwa wakati wa kikao cha bajeti kinachohudhuriwa na baraza la madiwani wa manispaa hiyo.
Akiwasilisha taarifa hiyo kwa niaba ya mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, mchumi wa manispaa ya Ilala, Ando Mwanduga amesema bajeti hiyo imepanda kutoka sh. bilioni 124 mwaka 2016/2017 hadi bilioni 287 kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Mwanduga amesema fedha hizo zimepatikana kwa makundi mawili ambapo la kwanza linajumuisha mapato ya ndani pamoja na fedha za ruzuku, lengo kuu likiwa ni kuendeleza miradi ya wananchi.
Aidha, Mwanduga amesema malengo makuu ya manispaa ya Ilala ni kuhakikisha wanakusanya mapato bila kumuumiza mwananchi ili kuhahakisha kiwango cha bajeti kinapanda ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Awali akiwasilisha mapendekezo ya bajeti hiyo mwenyekiti wa kamati ya uchumi na huduma za jamii, Jacob Kissi amesema kamati yake inakaribia kutumia bajeti ya sh. bilioni 122.9.
Ametaja baadhi ya miradi ya maendeleo itakayo itakayotekelezwa kuwa ni elimu ya msingi, ya sekondari, idara ya kilimo, umwagiliaji na ushirika, idara ya afya na ustawi wa jamii pamoja na idara ya maendeleo ya jamii na vijana.

No comments:

Post a Comment