Friday, 16 March 2018

Maofisa mawasiliano serikalini watakiwa kuwa mabalozi wa kodi
Richard Kayombo

MAOFISA Habari, Mawasiliano na Uhusiano serikalini wameombwa kuwa mabalozi wazuri katika sehemu zao za kazi na katika jamii wanayoishi kwa kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi.

Akizungumza wakati akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa kodi kwenye kikao kazi cha maofisa hao kinachomalizika leo jijini Arusha , Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, amesema elimu ya kodi itawafikia watu wengi zaidi kwa kuwa wengi wao wana ushirikiano mkubwa katika kutoa habari sahihi kwa umma.

“Kila mmoja wetu anachokifanya ni sauti kwa mwenzake mahali alipo, ndio maana hata katika mitandao mbalimbali tumekuwa tukisaidiana kwa kuwa, ukiona jambo baya linasemwa kuhusu taasisi ya mwenzako au serikali unamsaidia kutoa ufafanuzi, hivyo, mkielewa mada yangu hapa, najua mtanisaidia kuelimisha masuala ya kodi katika sehemu zenu za kazi na maeneo mengine”, amesema Kayombo.

Kayombo ameongeza kuwa, maofisa hao wana nafasi kubwa katika kuelimisha jamii na kusahihisha baadhi ya wananchi ambao wanakuwa na elimu isiyo sahihi kuhusu masuala yanayohusu kodi na ukusanyaji wa mapato kwa ujumla. 

Aidha, pamoja na mambo mengine, Kayombo amewakumbusha moafisa hao suala la kudai risiti kila wakati wanaponunua bidhaa ili kuchangia maendeleo ya nchi.

“Ni vizuri tu mkafahamu kuwa, tunasimamia kodi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kodi ya mapato na  ya ongezeko la thamani au kwa jina jingine kodi ya mlaji, ndio maana tunasisitiza kudai risiti kila mnapofanya manunuzi kwasababu usipopewa risiti na mfanyabiashara aliyesajiliwa kwa VAT na hata ambaye hajasajiliwa kwa VAT maana  yake unakuwa umemnufaisha yeye na familia yake,” amesisitiza Kayombo.

Amewaambia maafisa hao kuwa, wananchi wakidai risiti kila wanaponunua bidhaa mbalimbali, wanaepusha udanganyifu unaofanywa na wafanyabiashara wa kuficha mauzo halisi ambayo yanatumiwa na TRA kama sehemu mojawapo ya kuwakadiria kodi. Kikao kazi cha maofisa habari, mawasiliano na uhusiano serikalini kinatarajia inamalizika leo Machi 16.

No comments:

Post a Comment