Tuesday, 20 March 2018

Maofisa polisi Kenya wapunguziwa mishahara yao


MAOFISA waliomaliza masomo na walemavu wameanza kuacha nafasi mbalimbali baada ya Tume ya taifa ya huduma za Polisi kupunguza mishahara yao kwa kiwango cha asilimia 50 juma lililopita.
MaOfisa hao ambao tayari wamepokea mishahara yao ya mwezi Machi, wameliambia gazeti la The Nation la Jumapili kuwa, fedha zao zilikuwa zimepunguzwa, kwa wengine mpaka SH. 26,000 za Kenya.
Mabadiliko hayo yaliyowaathiri polisi walioanza kazi na walemavu yamefanyika mwezi huu, ingawa amri ilitolewa na mahakama kuitaka serikali kutotekeleza mpango huo .
Sheria inawasamehe kodi walio na ulemavu wanaopokea mshahara wa sh. za Kenya 150,000 na pungufu ya kiasi hicho.
Ujumbe unaoingia kwenye simu za maofisa hao unaonesha kuwa baadhi yao wanapata kiasi kidogo cha mpaka sh. 20 mwezi huu huku wengine wakiwa hawaambulii chochote. Suala hilo limewaudhi maofisa huku baadhi yao wakiwa tayari wameandika barua za kuacha kazi.
Mwenyekiti wa Tume ya Huduma kwa polisi, Johnstone Kavuludi amekanusha ripoti hiyo na kusema kwamba hakuna ofisa aliyekatwa wala kupunguziwa mshahara.
Kavuludi amewaambia wanahabari kwamba kilichofanywa ni kuhakikisha kila ofisa anapokea mshahara unaostahili.
“Kuna maofisa ambao hawajawasilisha vyeti vya kuhitimu stashahada na shahada lakini wanapokea mshahara wa ofisa wa cheo cha konstebo, hao ndio tunapambana nao,” amesema.
Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu, (KNCHR) Jumatatu imeshutumu vikali hatua hiyo ya kupunguzwa mishahara hiyo ya maaoisa wa polisi.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Kagwira Mbogori amesema idara ya polisi imekuwa ikitekeleza majukumu muhimu ya kudumisha amani na hatua hiyo itaathiri mno mageuzi ambayo yamekuwa yakiendelezwa na tume ya huduma kwa polisi.
“Sisi tunaangazia haki za maofisa hao jinsi tunavyoshughulikia raia wanaodhulumiwa. Kwa sasa tuna kesi kadhaa ambazo tunafuatilia kuhusu raia waliowavamia polisi kipindi cha kabla na baada ya uchaguzi,” amesema, kwa mujibu wa gazeti la Taifa Leo la Kenya.

No comments:

Post a Comment