Wednesday, 28 March 2018

Milioni 400 kujenga majengo manne ya kisasa Namtumbo


Moja ya majengo hayo

Mwandishi Wetu, Namtumbo

HALMASHAURI ya wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma imepokea sh. milioni 400 kutoka  ofisi ya Rais Tamisemi ili kuongeza majengo katika kituo cha afya Namtumbo.

Ofisa habari wa halmashauri hiyo, Yeremias Ngerangera amesema halmashauri hiyo ilipokea fedha hizo Novemba mwaka jana.

Amebainisha kuwa baada ya kupokelewa halmashauri ilipitia miongozo ya matumizi ya fedha hizo ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa.

Aidha, Ngerangera ameongeza kuwa baada ya kupitia miongozo ya matumizi ya fedha hizo, halmashauri imeanza ujenzi wa majengo hayo manne katika kituo cha afya Namtumbo kilichopo katika kata ya Rwinga.

Mhandisi wa majengo wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, Hasssani Kinonono amebainisha majengo yanayojengwa kuwa ni pamoja na lile la upasuaji, wodi ya kinamama wajawazito, maabara na nyumba ya waganga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, Christopher Kilungu amesema kutakuwa na ukarabati wa jengo la kuhifadhia maiti pamoja na kujenga kichomea taka kwa kutumia fedha zitakazo baki katika ujenzi wa majengo hayo manne.

Miongoni mwa majengo hayo

No comments:

Post a Comment