Friday, 23 March 2018

Mimba za utotoni changamoto inayohitaji ufumbuzi wa kudumu

Mariam Jumanne, Tanga

HALI ya mimba za utotoni hapa nchini imeendelea kuongezeka na hivyo kuwepo tishio kubwa la kumnyima mtoto wa kike haki yake ya msingi ya kupata elimu.

Akizungumza na wanafunzi wa shule sita za jiji la Tanga katika warsha ya siku moja kuhusu kampeni ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Mathias Haule amesema elimu ndio njia sahihi ya kutimiza ndoto za mtoto wa kike popote duniani.

Haule ameongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, wanafunzi 5,053 waliacha shule mwaka 2016 hapa nchini baada ya kupata ujauzito.

Amesema mimba 4,426 kwa mujibu wa takwimu hizo ni za wanafunzi wa shule za sekondari, na 627 ni za wasichana wa shule za msingi.

Aidha, amefafanua kuwa mikoa iliyoongoza kwa wanafunzi wengi kuacha shule kutokana na mimba ni Mbeya walitoka wanafunzi 380, Mwanza 372, Kilimanjaro 348, Dodoma308 na Ruvuma 300.

Haule ameongeza kuwa serikari imebaini sababu za mimba shuleni ni  pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu malezi chanya, umuhimu wa mtoto wa kike kusoma, mila na desturi na umaskini wa familia.

Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Tanga, Mwatumu Dossi amesema mwaka 2017 wanafunzi wa sekondari 20 walipata ujauzito katika mkoa huo.

Ametoa mwito kwa wazazi na walezi wa jiji la Tanga kuwa karibu na watoto wao ili kuwapatia elimu ya afya na jinsia ikiwemo kuacha kuwaoza wasichana katika umri mdogo.

Shule za msingi za jiji la Tanga zilizo shiriki kampeni ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni ni Changa, Juhudi, Chumbageni, Kisosora na shule binafsi ya Changa English Medium.

No comments:

Post a Comment