Thursday, 22 March 2018

Mkaa endelevu, mbao zaviingizia vijiji milioni 65/-


Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Uhifadhi wa Misitu ya Asili (TFCG), Charles Meshack akipanda mti siku ya uzinduzi wa mradi wa mkaa endelevu.

Seleman Kasei

WANAVIJIJI wa vijiji  vitatu vya Milingwa, Diguzi na Matuli kwenye halmashauri ya wilaya ya Morogoro vimefanikiwa kukusanya zaidi ya sh. milioni 65 kutokana na utunzaji wa misitu na uvunaji mkaa endelevu unaofanyika katika vijiji hivyo.

Meneja Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTFS), Charles Leonard amethibitisha hilo wakati akizungumza na wajumbe wa kamati ya madiwani ya maliasili na mipango na fedha wa halmashauri hiyo ambao walitembelea maeneo yanayojihusisha na utunzaji wa misitu na mkaa endelevu.

Amesema mapato hayo yamepatikana katika uvunaji ulioanza Oktoba mwaka jana ambapo wananchi wameonesha mwamko mkubwa.

Meneja huyo amesema mradi wa utunzaji misitu na mkaa endelevu umejikita katika kueendeleza misitu na kukuza uchumi wa wananchi wanaozunguka misitu ya asili.

Amesema mradi huo wenye lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo ya wananchi, unatekelezwa katika kata ya Matuli kwenye vijiji vitatu  vya Diguzi, Matuli na Lulongwe. Kata ya Tununguo vijiji vya Mlilingwa na Tununguo.

Meneja huyo amesema kwa muda mfupi wa mradi huo matokeo yamekuwa makubwa kwa wanakijiji wanaoshiriki wameinuka kiuchumi ikiwa ni kwa kupitia vikundi vya mikopo kama vicoba.

"Mradi wa TTFS unaofadhiliwa unaotekelezwa Shirika Uhifadhi Misitu Tanzania umekuwa chachu ya maendeleo kwani katika vijiji vitano zaidi ya sh. milioni 65 zimepatikana na kusaidia huduma za kijamii na washiriki," amesema.

Leonard amesema zaidi ya hekta 9,000 za msitu zinatunzwa na wanakijiji zaidi ya 700 ambao wamegawanyika katika makundi mbalimbali kama kuvuna mkaa endelevu, kilimo hifadhi, kupasua mbao na vikundi vya kukopeshana.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) Revocatus Njau amesema wao wanasisitiza wana jamii kutumia mkaa ambao unavunwa kwa uendelevu ili kutunza misitu.

Ametoa mfano misitu ya miombo itumike katika uvunaji wa mkaa endelevu ambayo imeonesha matokeo chanya ya kuchepua haraka tofauti na miti mingine.

"Naomba Serikali iandae Sera ya mkaa ili  iweze kuendana na sera nyingine kama ya misitu, nyuki na nishati nyingine kwani mkaa unategemewa na kundi kubwa na unaingizia taifa sh. trilioni 2.2 kwa mwaka na kutoka ajira kubwa," amesema.

No comments:

Post a Comment