Monday, 12 March 2018

Mkutano wa Trump na Kim Jong-Un waanza kuandaliwa


Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un (kushoto) na Rais wa Marekani Donald Trump.

UJUMBE wa Korea Kusini upo katika jitihada za maandalizi ya mkutano kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un.


Viongozi hao wa Korea Kusini wanatarajiwa kufika China na Japan kutoa maelezo kuhusu mkutano huo. Muda na mahali pa kufanyika mkutano huo bado hapajajulikana.
Viongozi wa juu wa Korea Kusini wiki iliyopita walifikisha ujumbe kwa Rais wa Marekan Donald Trump kuhusu nia ya kukutana na kufanya mazungumzo na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, huku Trump akikubali mara moja kushiriki katika mkutano huo na kuwapa taarifa China na mshirika wake Japan mara baada ya kupokea taarifa hizo. 
China imeonesha nia ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo lakini mahala pengine pa kufanyika mkutano huo pametajwa kuwa huenda ikawa ni Uswizi, Sweden ama Panmunjom.
Wakati huo huo viongozi wa usalama nchini Marekani wamesema wanajua hatari iliyoko katika mkutano huo lakini wamefurahishwa na hatua ya Trump kukubali kushiriki.
Mkurugenzi wa CIA Mike Pompeo amesema anajua ugumu wa kujihusisha na Korea Kaskazini, lakini ana amini kuwa Trump amekubali kushiriki mazungumzo hayo kwa ajili ya kuondoa matatizo na Korea Kaskazini na si vinginevyo.
''Hiki ni kitu ambacho kimepiganiwa kwa miongo kadhaa sasa, na wakati huo huo amekubali kuzungumza kuhusu mpango wa kusitisha Nuklia, mwisho itajulikana kuwa sio maneno tuu au nani amesema nini, uongozi huu uko makini na wakati wote wa mazungumzo shinikizo kuhusu ya Korea Kaskazini litaendelea, hakuna kupumpuzika hadi rais ahakikishe amefikia malengo aliyoyaweka katika kipindi atakacho kuwa madarakani,'' amesema Mike Pompeo.
Aidha, Trump amesema mkutano huo utaleta matokeo makubwa kwa dunia. Lakini wakosoaji wa siasa za Marekani wamesema mazungumzo hayo yakienda vibaya basi nchi hizo mbili zitakua na uhusiano mbovu zaidi.

No comments:

Post a Comment