Thursday, 8 March 2018

Mtasingwa kuiwakilisha Tanzania UNCSWSuleiman Kasei

MSICHANA wa Kitanzania, Helga Mtasingwa kutoka Chama cha Girl Guides Tanzania (TGGA), amechaguliwa na Chama Girl Guides na Girl Scouts Duniania (WAGGGS), kuwakilisha nchi katika Mkutano wa 62 wa Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Wanawake Duniani (UNCSW).

Akizungumza na wanahabari leo kabla ya kuondoka kuelekea Marekani katika mkutano huo, Mtasingwa amesema atatumia mkutano huo ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Wanawake (UN Womens ) kuwakilisha changamoto zinazowakabili watoto wa kike wa Kitanzania.

Amesema nafasi ya kuwakilisha TGGA ataitumia vema ili iweze kutoka matokeo chanya kwa nchi na wasichana kwa ujumla.

Mtasingwa amebainisha kuwa watoto wa kike wa Tanzania wanakabiliwa na changamoto za kupata elimu  bora, huduma za afya na ukosefu wa usalama wa usafiri katika kundi hilo.

"Tumechaguliwa watoto wa kike 12 duniani kote, Tanzania nipo peke yangu kushiriki mkutano wa 62 wa Tume ya UN kuhusu hali ya wanawake duniani, nitatumia mkutano huo kuwasilisha changamoto anazokutana nazo mtoto wa kike nchini," amesema.

Mtasingwa amesema maandalizi aliyofanyiwa na TGGA baada ya kuchaguliwa kuwa mwakilishi yamemjengea ujasiri, kujiamini, uthubutu wa kusimamia hoja hivyo ni matumaini yake uwakilishi wake utakuwa na matokeo chanya.

Kwa upande wake Kamishna wa Kimataifa wa TGGA, Miryam Mjema alimtaka Mtasingwa kuiwakilisha Tanzania vizuri katika mkutano huo kwa kuyasema yote ambayo yanarudisha nyuma jitihada za mtoto wa kike.

Katibu wa TGGA, Grace Shaba amesema chama hicho kimejipanga kuwafikia watoto wengi kwa kuwapatia elimu ya umuhimu wa kujiunga nao.

Shaba amesema kwa sasa TGGA ina wanachama hai 147,000 katika mikoa 23 ambapo kwa mwaka huu wanatarajia kumalizia mikoa mitatu ya Kigoma, Kagera na Geita.

No comments:

Post a Comment