Saturday, 10 March 2018

Muda kuwania tuzo ya maji waongezwa


Maeneo mengi nchini yanakabiliwa na ukame, hivyo familia zinatumia muda mrefu kusaka maji kwa matumizi mbalimbali

SHIRIKA lisilo la kiserikali ‘Shahidi wa Maji’ kwa kushirikiana na wadau wengine nchini kupitia programu yake ya Uhakika wa Maji, limeongeza muda wa uwasilishwaji machapisho na programu za redio na runinga kutoka kwa wanahabari na vyombo vya habari wanaowania tuzo ya uandishi wa habari za maji.

Tuzo hizo zilizinduliwa  na Shahidi wa Maji pamoja na washirika wake kwa mara ya kwanza Juni mwaka 2017, na kupewa jina la ‘Tuzo ya Habari za Maji.

Ili kushiriki katika tuzo hiyo, waandishi wanatapaswa kuwasilisha kazi  walizochapisha au walizorusha katika vyombo mbalimbali vya habari zinazohusu suala mtambuka la maji.

Kazi hizo zinatakiwa zihusu usimamizi na utawala wa rasilimali maji, ukame, mafuriko, usambazaji maji, uchafuzi wa mito na vyanzo vya maji.

Vyombo vya habari pamoja na waandishi watakaoshinda tuzo hizo watapata zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu, vifaa vya kuboresha ufanisi wa kazi kama vile kamera na kompyuta mpakato, kombe la tuzo pamoja na vyeti vya ushiriki.

Lengo ni kuboresha uwajibikaji miongoni wa wadau wa sekta ya habari katika kuchapa na kusambaza habari zinazohusu maji ili kuleta mabadiliko chanya.

Pia, makala za washindi  zitapata fursa ya kurushwa kwenye tovuti za shirika au kusambazwa katika vyomba mbalimbali vya habari na mitandao ya kimataifa kama: BBC, UK Guardian, Circle of Blue and Ooska News ambayo ni nafasi na fursa ya kipekee kwa waandishi na vyombo vya habari kusomwa zaidi na kutambuliwa kwa mchango wao katika kusaidia kuboresha sekta ya maji nchini.
Tuzo hizo zimeandaliwa mahsusi kwa wanahabari na vyombo vya habari ambavyo vinatoa taarifa kuhusu masuala ya maji na kuchochea mabadiliko chanya katika uwajibikaji wa wadau wa sekta ya maji.  

Shahidi wa Maji na washirika wake imejikita kufanya kazi ili kubadilisha namna ambayo rasilimali maji inasimamiwa kwa manufaa ya wananchi wote, mazingira na uchumi wa nchi.

Mwisho wa uwasilishaji wa kazi za wanahabari na vyombo vya habari ni Mei 31, mwaka huu.


No comments:

Post a Comment