Friday, 16 March 2018

Mugabe adai hakutegemea Mnangagwa angemwondoa madarakani


Robert Mugabe
ALIYEKUWA Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe amevunja ukimya kwa mara ya kwanza tangu aondolewe madarakani, amesema amekua muhanga wa mapinduzi ya kijeshi.
Akizungumza na televisheni ya SABC ya Afrika Kusini, Mugabe amesema Rais wa sasa Emerson Mnangagwa asingeweza kuingia madarakani bila jeshi kuingilia kati.
Akiwa katika nyumba yake ya kifahari mjini Harare, Mugabe amekemea mbinu zilizotumika kumuondoa madarakani.
Amesema alikuwa tayari kufanya mazungumzo na Rais wa sasa Emerson Mnangagwa na angehakikisha mabadiliko ya madaraka ya uhalali na si yale ya kulazimishwa.
Mugabe amesema kuwa yuko tayari kwa ajili ya mazugumzo na Mnangagwa ili kulinda katiba yao.
Hakuna uhakika kama rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 94 iwapo anataka kurudi madarakani ama la, lakini ni wazi kuwa anadhani amesalitiwa na Mnangagwa rais wa sasa wa taifa hilo.
Amesema hakudhani kama angepoteza imani yake kwa Mnangagwa kwani yeye ndiye alimsaidia kuingia serikalini.
“Siamini kama yeye Mnangagwa angeweza kuniondoa madaraki , nimemuingiza serikalini, nimemsaidia alipokua jela anataka kunyongwa, sikuwaza kabisa kama siku moja ndiye atakuwa mtu wa kunitoa madarakani,” amesema Mugabe.
Aidha, Mugabe ameongeza kuwa Rais Mnangagwa ameingia madarakani kwa njia zisizo halali.
“Lazima tufute aibu hii, ambayo tumejiletea wenyewe, hatuistahili, hatuistahili, hatuistahili , tafadhali hatuistahili kabisa.Tunatakiwa kuwa nchi inayoheshimu katiba, ndiyo tunaweza kuwa na mapungufu hapa na pale lakini bado lazima tuheshimu sheria,” amesema Mugabe.
Katika mitandao mbalimbali ya kijamii, baadhi ya wazimbabwe wanashangazwa na mkongwe huyo wa miaka 94 kutoa kauli huku wengine wanaamini kuwa amepoteza uhalisia kabisa baada ya kuongoza kwa miaka 38 , wakati wake sasa umekwisha.

No comments:

Post a Comment