Thursday, 1 March 2018

Museveni aagiza uchunguzi wa vinasaba baada ya mauaji, awaita wauaji nguruwe


RAIS wa Uganda Yoweri Museveni ameagiza kuanzishwa uratibu wa vinasaba nchini humo baada ya mauaji ya kushtua kutokea.
Amesema uratibu huo wa taifa utakaokuwa na taarifa za kielektroniki utarahisisha kukamatwa kwa wahalifu.
Museveni ametoa malekezo ya namna uratibu huo utakavyo fanya kazi katika mtandao wa Twitter.
Ni baada ya mauaji ya msichana mwenye umri wa miaka 28 , Susan Magara, ambaye kifo chake kimegusa taifa zima.
Magara alitekwa Februari 7, mwaka huu, na wateka nyara wakadai kikombozi cha dola za Kimarekani 16,200. Mwili wake uligundulika Jumatatu jijini Kampala.
Museveni ameelezea namna uratibu huo wa vinasaba ungefanya kazi: “Ili kuwatokomeza wahalifu, inabidi tuitazame kwa namna mbili:
“Kuchukua alama za kiganja cha kila mtu na kuchukua vinasaba vya kila mtu. Kuna wale watakaobishia kwamba kuchukua vinasaba vya kila mtu siyo demokrasia. Sielewi kwanini sio demokrasia.
"Rekodi za vinasaba vya kila mtu ni jambo zuri ukilinganisha na sampuli ya damu, au mbegu za kiume au jasho linalopatikana kwenye eneo la tukio. Alama za kiganja ni bora zaidi kuliko alama za kidole gumba sababu mhalifu anaweza kuacha alama hizo lakini asiache ya kidole." Pia aliwaita wahalifu hao "nguruwe"
“Mauaji ya Susan yanaonesha aina ya nguruwe tulionao Afrika ambao hawathamini hazina ya wazuri kama Suzzie ambaye sikuwa na bahati ya kuonana naye.
Mwaka jana , watu 12 walifikishwa mahakamani nchini Uganda kwa mashtaka ya mauaji ya wanawake tisa katika eneo la kaskazini nje ya mji mkuu Kampala.
Jumla ya wanawake 19 wameuawa katika maeneo ya mji wa Kampala tangu mwezi Mei, 2017.
Wengi kati ya hao walikuwa wamebakwa na kukatwa viungo vyao, huku miili yao ikiachwa porini na pembezoni mwa barabara.

Mkuu wa polisi nchini Uganda alisema imani za kishirikina zinahusishwa katika baadhi ya mauaji.

No comments:

Post a Comment