Josephine Majani
MAHAKAMA Kuu nchini Kenya imeamuru mwanamke Josephine Majani aliyeteswa na kudhalilishwa wakati
wa kujifungua hospitalini, alipwe fidia ya dola 25,000 za Marekani.
Mwanamke huyo
alidhalilishwa miaka mitano iliyopita katika kisa ambacho kilizua malalamiko kutoka
kwa raia na watetezi wa haki za kibinadamu baada ya kuangaziwa kwenye vyombo
vya habari na mtandaoni.
Jaji wa
mahakama kuu ya Bungoma, magharibi mwa Kenya, Abida Aroni amesema mamlaka ya
afya nchini Kenya ilikiuka haki za msingi za Josephine Majani alipotengwa na
kukosa kuhudumiwa wakati wa kujifungua katika hosipitali ya umma mwaka 2013.
Jaji huyo amesema
haki ya msingi ya afya ya Majani, pamoja na heshima yake vilikiukwa kupitia
yeye kuteswa kimwili na kutusiwa na wauguzi katika hospitali ya Bungoma.
Na kutokana na
hilo, akaamuru alipwe fidia ya dola 25,000. Majani amefurahia uamuzi huo akisema
hatimaye haki imetendeka.
Aliyoyapitia
Josephine mikononi mwa wauguzi hao yalijulikana baada ya mtu kurekodi video
kwenye simu yake na kuipakia kwenye mtandao wa kijamii.
Martin Onyango,
wakili wa Josphine kutoka kituo cha Afrika kuhusu afya ya uzazi anasema kesi
hiyo ni ushindi mkubwa kwa wanawake wanaotafuta huduma bora za afya ya uzazi
katika hospitali za umma nchini Kenya.
Mwandishi wa
BBC Victor Kenani aliyeko Nairobi anasema visa vinavyohusiana na unyanyasaji
vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara katika hospitali za umma nchini Kenya.
Majani amesema
fidia hiyo itamsaidia kumlea mtoto ambaye karibu ampoteze wakati wa kujifungua.
Kwa mujibu wa
shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu idadi ya watu, wanawake 495 kati ya laki
moja walio wajawazito hufa kila mwaka kutokana na matatizo wakati wa
kujifungua.
Shirika hilo
linasema uamuzi wa leo umetoa mwongozo kuwa lazima wapewe huduma ya kujifungua
ya viwango vya juu ili kuzuia vifo vya aina hiyo kutoka.
Chanzo:
BBC
No comments:
Post a Comment