Friday, 9 March 2018

Mwanamume aliyepasuliwa ubongo kimakosa azungumza


Hospitali Kuu ya Kenyatta
MWANAUME aliyefanyiwa upasuaji wa ubongo kimakosa nchini Kenya ameruhusiwa kuondoka hospitalini na kuzungumzia masaibu yaliyompata.
Akiwa na alama kubwa kichwani, Samwel Kimani aliiambia televisheni ya NTV kuwa, alikuwa amepoteza fahamu wakati alilazwa hospitalini na hakufahamua kilichosababisha madaktari kumfanyia upasuaji.
Hospitali ya Kenyatta iliomba msamaha baada ya kukiri kuwa vifaa vya kutambua wagonjwa hao wawili vilikuwa vimechanganyika.
Mwanamume ambaye alistahili kufanyiwa upasuaji wa ubongo baada ya kuganda kwa damu naye aliruhusiwa kurudi nyumbani lakini bado haijulikani ikiwa anahitaji kufanyiwa upasuaji huo.
Kisa hicho kimewashangaza wakenya wengi tangu kiibuke na kilisababisha Ofisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Kenyatta nchini humo kwenda likizo ya lazima.
Hatua ya kumtuma Lilly Koros kwenye likizo ya lazima ilitangazwa na Waziri wa Afya wa nchi hiyo, Sicily Kariuki ambaye amesema hatua hiyo ilikusudia kupisha uchunguzi.
Mmoja kati yao wagonjwa hao ndiye alihitaji upasuaji wa kichwa ili kuondoa damu iliyokuwa imeganda kwenye ubongo wake.
Huyo mwingine alikuwa amefura kwenye kichwa lakini alihitaji matibabu ambayo hayakushirikisha upasuaji.
Lakini asiyehitaji upasuaji ndiye aliyeishia kufanyiwa upasuaji. Madaktari waligundua kosa hilo saa chache baada yao kuanza upasuaji walipogundua kwamba hawakuweza kuiona damu iliyoganda kwenye ubongo wa mgonjwa waliyekuwa wanamfanyia upasuaji huo.

No comments:

Post a Comment