Friday, 9 March 2018

Mwandishi Uganda ashinda tuzo kubwa ya uandishi duniani


Jennifer Nansubuga Makumbi

MWANDISHI Jennifer Nansubuga Makumbi ambaye Uingereza ilikataa kuchapa riwaya zake, ameshinda moja ya tuzo kubwa kabisa za uandishi duniani.

Jennifer mwandishi wa Uganda ambaye makazi yake sasa yapo Manchester Uingereza, amejishindia moja ya tuzo kubwa kabisa duniani ya uandishi. Alitoka nchini Uganda miaka 17 iliyopita na kuhamia Uingereza .
Makumbi ameweza kujishindia tuzo za Windham Campbell yenye thamani ya dola 165,000 kutoka chuo kikuu cha Yale kilichopo nchini Marekani.
Amesema ushindi huu umemshangaza ingawa huwa anafanya kila kitu muhimu katika uandishi wake. Mwandishi huyo anasema kiasi hicho cha fedha ni muda mrefu umepita hajawahi kukishika.
Fedha iliyotolewa katika tuzo hii ni mara mbili ya kiasi cha fedha kinachotolewa kwa mshindi wa Booker Prize na waandaaji wanasema tuzo hii ni kubwa zaidi katika uandishi wa vitabu baada ya Noble Prize.
Makumbi ni mmoja kati ya washindi wanane waliopokea tuzo za Windham Campbell kwa mwaka huu katika uandishi wa riwaya za kubuni,uhalisia, maigizo na ushairi na yeye ni mshindi pekee aliyechapisha kazi moja kamili ya muda mrefu.
Waandishi wengine kutoka Uingereza waliokuwa kwenye orodha wote wakiwa wanaandika simulizi zenye uhalisia walikuwa ni Sarah Bakewell na Olivia Laing.
Tuzo hizo zilizoanzishwa na Donald Windham na kubeba jina lake pamoja na mshirika wake Sandy M Campbell na tuzo za kwanza zilianza kutolewa mwaka 2013 na kuwapa waandishi fursa ya kuzingatia kazi zao wakiwa huru bila changamoto za kifedha.
Makumbi anasema taarifa hii ya kupata tuzo hakuitarajia kwa kuwa inaandaliwa na wamarekani na kwa kawaida huwa wanapata vitabu vingi, "Ninashangaa kuwa miongoni mwa washindi,"amesema.
Toleo la riwaya yake ya kwanza, Makumbi aliichapisha nchini Kenya miaka minne baada ya wachapishaji wa Uingereza kukataa kuchapisha kitabu chake cha "Too African" na baadaye Januari mwaka huu kitabu hicho kilizinduliwa nchini Uingereza.
Mwandishi amesema wachapishaji na wasomaji wa Uingereza wanapenda kusoma vitu ambavyo vinaendana na tamaduni zao za Ulaya au ambazo wamezizoea hata kama wanasoma simulizi kuhusu Afrika.
Lakini amekielezea kitabu cha" Kintu" kuwa kinazungumzia Uafrika halisi. Kitabu hiki kimeangazia hadithi ya simulizi za famila moja ya Uganda ambayo waliamini kuwa walilaaniwa kwa zaidi ya miaka 250.
Mwandishi huyo anasema namna ambavyo ameandika kitabu chake wasomaji walikuwa hawajauzoea ila sasa anaamini wataanza kumuelewa.
Kama ninataka kuitambulisha Afrika lazima niieleze katika mrengo wa kiafrika badala ya kuwaambia vitu ambavyo natarajia kuwa wanavijua.

No comments:

Post a Comment