Saturday, 10 March 2018

Mwenyekiti wa kijiji auawa kwa kukatwa mapanga


Suleiman Kasei

MWENYEKITI wa kijiji cha Nyarugusu, kata ya Heru Ushingo, wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, Aramu Kaigwe 48, (NCCR-Mageuzi) ameuawa kikatili  kwa kukatwakatwa mapanga.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Juju Danda amekiri kutokea mauaji hayo ya kikatili yanayodaiwa kutekelezwa na watu wasiojulikana.

“Habari hizi ni za kweli mwenyekiti wetu ameuawa huko Kasulu vijijini na kwa sasa chama kinaendelea na mchakato wa kuhakikisha anahifadhiwa,” amesema.

Diwani wa kata ya Heru Ushingo, Banka Jwijwi, amesema marehemu Aramu aliuawa usiku wa kuamkia Alhamisi ya wiki hii akiwa kazini kwake.

Jwijwi  amesema marehemu alikuwa mlinzi ambapo tukio la kuuawa lilitokea ila mwili wake ulitupwa katika pori lilipo pembezoni mwa kijiji.

"Tukio hili limetusikitisha sana sisi wanakijiji kwani marehemu alikuwa mtu wa watu na hakuna taarifa yoyote ya kuwa alikuwa ametofautiana na mtu hali ambayo inatuacha na majonzi makubwa,” amesema.

Ameongeza kuwa taarifa za kifo zilijulikana baada ya mkewe kumtafuta kupitia simu bila mafanikio siku ya Alhamisi hivyo aliwasiliana na ndugu zake na kuanza kumtafua ambapo walikuja kumkuta katika pori hilo akiwa amekatwakatwa na mapanga.

Diwani huyo alisema tukio hilo limeripotiwa katika kituo cha Polisi kilichopo katika Kambi ya Nyarugusu na baadaye cha wilaya ya Kilosa ambapo jana waliwaruhusu kumzika.

Kwa mujibu wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema taarifa alizopata kwa watu wake wa karibuni wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Zitto amesema ni la kusikitisha hasa katika mkoa huo na medani za kisiasa huku akilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha watu waliofanya tukio hilo wanapatikana.

“Natoa pole kwa chama cha NCCR-Mageuzi na wananchi wote wa Kasulu kwa tukio hili baya zaidi ambalo limetokea kwa kuuawa kiongozi wao,” amesema.

Matukio ya wanasiasa na wananchi kutekwa yamekuwa yakitokea kwa kasi ambayo haikuzoeleka katika nchi hapo awali hali ambayo inatia hofu kubwa miongoni mwa jamii katika maeneo mengi nchini.

No comments:

Post a Comment