Sunday, 25 March 2018

Mwigulu: Inapobidi walimu wachapeni viboko wanafunzi kuwafunza maadili

Dk. Mwigulu Nchemba (mwenye tai yenye rangi ya bendera ya taifa) akiwa amezungukwa na wanafunzi alipowasili katika shule ya sekondari Lulumba. 

WAZIRI wa Mambo ya ndani, Dk.  Mwigulu Nchemba amewataka walimu kuendelea kutoa elimu bora kwa wanafunzi kwa kuwafundisha maadili mema na inapobidi matumizi ya fimbo yatumike.

Akizungumza katika harambee ya ujenzi wa mabweni ya shule ya sekondari  Lulumba wilaya ya Iramba mkoani Singida, jana, Dk. Nchemba alisema walimu wanatumia fimbo kunyoosha nidhamu za wanafunzi ili kutengeneza hatma ya nchi.

“Kuna wakati walimu wananyoosha nidhamu za wanafunzi lakini ninyi hamuoni hii na kulalamika tu, kinachofanyika ni kwa manufaa yetu…niwaombe kwenye kutumia mifano tumieni mifano na kwenye kutumia fimbo fanyeni hivyo ili kutengeneza taswira ya nchi yetu,” amesema.

Amesisitiza kuwa ni lazima kuendelea kulinda hadhi za walimu kwa kuwapatia miundombinu bora ya ofisi na vyumba vya madarasa.

Amesema majengo ya taasisi yanapaswa kuwa bora zaidi na sio kutumia ramani za awali pekee kwani zinapaswa kuboreshwa kulingana na maendeleo yaliyopo.

“Naunga mkono ujenzi huu wa mabweni ya wanafunzi, ukarabati wa vyumba vya madarasa na ofisi za walimu hivyo nachangia mifuko 200 ya saruji nawaahidi pia kutoa sh. milioni sita,” amesema.

Mkuu wa wilaya Iramba, Emmanuel Luhaula amesema shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma kutokana na umahiri wa walimu kwani watoto hao wanajua kujieleza kama wanasoma chuo kikuu.

Amesema wananchi wa Iramba wanatakiwa kujivunia  kuwa na shule zao pamoja na walimu hao ili kuboresha elimu wilayani humo.

“Tunafanya jitihada ili kuhakikisha kila sekondari kunajengwa mabweni ili kuondoa kero ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shule.Sisi wa Iramba tushindwe wenyewe kukutumia. Nimekuwa mbunge lakini anayoyafanya mbunge huyu Mimi sikuyafanya,” amesema Luhaula.

Naye, Mkuu wa shule hiyo, Jeremiah Kitiku amesema licha ya kufanya vizuri kitaaluma, wanakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa baadhi ya majengo, upungufu wa vitabu vya masomo ya kiada 274.

“Mahitaji ya vitabu vya kiada ni 2,802 vilivyopo 2,328 upungufu ni 274. Pia tunachangamoto ya kutokuwa na uzio kwa usalama wa wanafunzi, walimu na mali za shule,” amesema Kitiku

Hata hivyo, amesema malengo ya shule hiyo ni kukarabati vyumba tisa vya madarasa na  ofisi nane za walimu ambazo zitagharimu sh. milioni 169.4.

Katika harambee hiyo, saruji iliyokusanywa ni mifuko 209, ahadi  ya fedha ni 8,486,000, ahadi ya mifuko ya saruji 572, Gypsum 50 na  nondo tani moja na hivyo kufanya ahadi na fedha taslimu kuwa ni 19,494,300.

No comments:

Post a Comment