Wednesday, 21 March 2018

Nditiye acharuka atoa siku 14 kwa UCSAF kuleta ripoti ya mawasiliano Pemba


Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa ziara yake kwa taasisi za mawasiliano Zanzibar. Kushoto ni Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika hilo, Hassan Mwang’ombe na kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL), Hussein Selemani Nguvu.Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye ameupa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wiki mbili kwenda Pemba kukagua hali ya mawasiliano ya simu za mkononi na kuwasilisha taarifa hiyo ofisini kwake.

Mhandisi Nditiye ametoa agizo hilo akiwa kwenye ziara yake ya kikazi Zanzibar ya kukagua hali ya mawasiliano kisiwani humo na kutembelea taasisi za mawasiliano zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambapo suala la mawasiliano ni la muungano.

Nditiye amesema amepokea taarifa kutoka kwa wabunge wa Kisiwa cha Zanzibar kuwa hali ya mawasiliano kwenye kisiwa hicho sio nzuri na sehemu nyingine hakuna mawasiliano kabisa licha ya kuwa kuna minara ambayo inatoa huduma za mawasiliano.

Amesema ameambiwa kutokana na jiografia ya Pemba ambapo kuna milima na mabonde hivyo mawasiliano si ya uhakika. “Nawaagiza muende Pemba mkaainishe maeneo yote ambayo hayana mawasiliano na muwasilishe taarifa hiyo ofisini kwangu baada ya wiki mbili,” amesema Mhandisi Nditiye.

Meneja Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ,Ofisi ya Zanzibar Esuvatie-Aisa Masinga wakati akiwasilisha taarifa yake kwa Mhandisi Nditiye kuhusu majukumu ya ofisi yake ya usimamimizi na udhibiti wa mawasiliano na posta, amekiri kuwa yapo baadhi ya maeneo Pemba na Unguja ambapo hali ya mawasiliano sio nzuri na hairidhishi.

Ameongeza kuwa Pemba kuna maeneo ambayo hakuna mtoa huduma na pale ambapo mawasiliano yapo bado ubora wa huduma sio mzuri. Pia ameyataja maeneo yasiyo na mawasiliano kwa upande wa Mkoani kuwa ni Kengeja na Chokochoko na kwa upande wa Micheweni ni Konde na Gando.

Amefafanua kuwa sehemu nyingine za Pemba mtandao wa Zantel upo lakini ‘coverage yake’ sio nzuri. “Ili kufanya mawasiliano yawe mazuri kwa Pemba, ni muhimu ‘site’ zikaongezwa hasa ukizingatia hali ya kijiografia ya kisiwa hicho,” amesema Masinga. Mawasiliano ya kisiwa cha Pemba hayaridhishi, tunapendekeza Serikali kupitia UCSAF kuweka minara sehemu ambazo hakuna mawasiliano.

Naye mwakilishi wa UCSAF, John Munkondya amepokea maelekezo ya Mhandisi Nditiye ambapo mfuko huo utakwenda Pemba kukagua hali ya mawasiliano na kuwasilisha ripoti ofisini kwake ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata mawasiliano ya uhakika.

“Sisi kama UCSAF tumechukua taarifa hii ya maeneo ambayo hayana mawasiliano, tutakwenda Pemba kukagua na maeneo hayo yataingizwa kwenye utaratibu wa kanda maalumu ili tuweze kufikisha mawasiliano,” amesema Munkondya.

No comments:

Post a Comment