Monday, 12 March 2018

Nkurunzinza naye atangazwa kuwa kiongozi wa maisha


Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza
CHAMA tawala nchini Burundi CNDD/FDD kimemtangaza Rais Pierre Nkurunzinza kama kiongozi wa milele ndani ya chama hicho.
Uamzi huo umefikiwa baada ya vikao vya siku tatu vya mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika katika eneo la Buye alikozaliwa Nkurunziza Kaskazini mwa nchi hiyo.
Uamuzi huo pia unachukuliwa wakati Burundi inajiandaa kufanya marekebisho ya Katiba ili kumruhusu Rais Nkurunzinza kuendelelea kuongoza taifa hilo hadi mwaka 2034.
Taaarifa fupi ya chama cha CNDD/FDD imesema vikao hivyo vilinuia kuimarisha chama tawala na taasisi zake.
Lakini pia chama hicho tawala kimechukua uamuzi wa kumuongezea hadhi na kumpa cheo cha juu Rais Nkurunziza na hivyo kumtangaza kuwa ni kiongozi mkuu wa kudumu ndani ya chama.
Kwenye hafla na makundi ya utamaduni ya chama tawala, katibu mkuu wa CNDD/FDD, Evariste Ndayishimiye aliutangazia umati azimio hilo aloliitaka kuwa ni muhimu mno katika uhai wa chama tawala.
Tangazo hilo la CNDD/FDD kumfanya Rais Nkurunzinza kama Kiongozi Mkuu wa Kudumu linajiri wakati Burundi inajiandaa kwa kura ya maoni kuhusu Marekebisho ya Katiba baadaye mwezi Mei. Kati ya mambo mengi katiba hiyo ikipitishwa itamuwezesha Rais Nkurunzinza kuweza kuwania Urais mpaka mwaka wa 2034.
Wadadisi wengi wa siasa za Burundi wanaamini kuwa hatua hii ya chama tawala inanuia kumaliza haraka mjadala wa mtetezi wa kiti cha Urais kwa niaba ya chama hicho na kuonesha mustakabali wa uongozi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2020.
Lakini pia uamzi huo unapeleka ujumbe kwa wafuasi wa CNDD/FDD na haswa viongozi wenye nia pengine ya kuwania nafasi hiyo na hivyo kujaribu kukiepusha chama tawala na mpasuko kama ilivyotokea mwaka wa 2015 katika mzozo kuhusu muhula wa sasa wa Rais Nkurunzinza.
Isitoshe kwa wachanganuzi wa siasa bado wanaiona hatua hii ya Rais Nkurunziza kutangazwa kiongozi wa maisha kama dalili tosha ya jinsi kiongozi huyo alivyokidhibiti chama cha CNDD/FDD.
Hatua iliyofanywa na CNDD/FDD ya kuidhinisha Nkurunziza kusalia madarakani ni sawa na ile iliyofanywa na Chama tawala cha National People's Congress cha China ambapo kimeidhinisha marekebisho ya kipengele cha Katiba na kumfanya Rais Xi Jinping wa nchi hiyo kusalia mamlakani hata baada ya muhula wake wa pili kumalizika hapo mwaka 2023.

No comments:

Post a Comment