Friday, 23 March 2018

Polisi yaahidi kudhibiti mtandao wa dawa za kulevya ZanzibarMkuu wa Operesheni Maalum za Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Liberatus Sabas (kulia), akizungumza na Kamanda wa Polisi mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna msaidizi wa Polisi (ACP ), Hasina Tawfiqi wakati wa operesheni maalum ya kukabililiana na mtandao wa dawa za kulevya na uhalifu dhidi ya watalii inayoendelea katika mikoa ya Zanzibar.

Mwandishi Wetu, Zanzibar

JESHI la Polisi nchini limesema operesheni ya kukabiliana na mtandao wa dawa za kulevya katika Visiwa vya Zanzibar itaendelea sanjari na kuwadhibiti wahalifu wanaofanya vitendo vya kuwaibia na kuwadhuru watalii jambo ambalo linatia doa usalama uliopo katika visiwa hivyo.

Mkuu wa operesheni maalum za Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi DCP Liberatus Sabas yupo Zanzibar akiongoza timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, pamoja na Kamisheni ya Polisi Zanzibar kwa lengo la kuongeza nguvu katika kuzuia na kupambana na mtandao wa dawa za kulevya pamoja na uhalifu dhidi ya watalii.

DCP Sabas amesema operesheni hiyo haitawaacha salam wahalifu hao kwa kuwa inafanyika kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha haimwachi mhalifu anayejihusisha na vitendo hivyo viovu vinavyochafua taswira nzuri ya usalama.

“Operesheni hii ni endelevu na niwape tu salamu wahalifu kuwa jambo la msingi ni wao wenyewe kujisalimisha kwa kuwa awamu hii hata wakikimbia tutawasaka na kuwakamata  kwa kuwa nguvu ipo na tunapata ushirikiano kwa wananchi wema wanaochukia vitendo vya uhalifu,” amesema Sabas.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kamishna msaidizi wa Polisi, Hasina Tawfiqi amesema katika operesheni hiyo wamefanikiwa kukamata dawa za kulevya aina ya Heroin kete 695 sawa na ujazo wa gramu 31.3 pamoja na watuhumiwa 21.

Amewasihi wakazi wa Kaskazini Unguja na mikoa jirani kuendelea kutoa taarifa ili kuweza kukomesha mtandao wa biashara hiyo pamoja na kuhakikisha kuwa watalii wanaotembelea mkoa huo wanafanya kazi zao kwa amani na usalama.

Operesheni hiyo pia imefanyika katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo watuhumiwa 58 walikamatwa pamoja na dawa za kulevya aina heroin kete 1293 na vifuko vitatu sawa na gramu 74.385.

No comments:

Post a Comment