Tuesday, 20 March 2018

Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy adaiwa kupata msaada wa Gaddafi


Nicolas Sarkozy

ALIYEKUWA Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy anazuiliwa na polisi akihojiwa kuhusu tuhuma kwamba alipokea fedha za kufadhili kampeni zake kutoka kwa kiongozi wa zamani wa Libya Kanali Muammar Gaddafi.
Polisi wanachunguza tuhuma hizo kuhusiana na ufadhili wa fedha alizotumia kwenye kampeni za uchaguzi wa urais mwaka 2007.
Polisi waliwahi kumhoji awali.
Msaidizi wake wa zamani Alexandre Djouhri pia alikamatwa jijini London hivi karibuni. Sarkozy alishindwa katika juhudi zake za kutaka kurejea madarakani mwaka 2012.
Duru kutoka mahakamani zimesema rais huyo wa zamani alikuwa anahojiwa Nanterre, magharibi mwa Paris. Mwaka 2013, Ufaransa ilianzisha uchunguzi kuhusu tuhuma kwamba kampeni ya Sarkozy ilipokea mchango kutoka kwa hazina ya fedha haramu za Gaddafi.
Sarkozy anakanusha tuhuma hizo. Duru zinasema mmoja wa mawaziri wa zamani wa Sarkozy na ambaye ni mshirika wake wa karibu Brice Hortefeux pia alihojiwa na polisi Jumanne.
Tuhuma hizo zilitolewa na mfanyabiashara Mfaransa mwenye asili ya Lebanon Ziad Takieddine na baadhi ya maofisa wa zamani wa Gaddafi.

No comments:

Post a Comment