Saturday, 31 March 2018

RDO yapongezwa kwa kufanikisha mradi wa maji


Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza akimtwisha ndoo ya maji mmoja ya wa kinamama waliohudhulia uzinduzi wa mradi wa maji ulifadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la Rural Development Organization (RDO), Tanzania.

Mwandishi Wetu, Iringa

SHIRIKA lisilo la kiserikali Rural Development Organization (RDO) Tanzania limepongezwa kwa kufanikisha upatikanaji wa maji katika baadhi ya vijiji vya wilaya ya Kilolo na Mufindi.

Pongezi hizo zimetolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Ndala ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo itachochea maendeleo kwa wananchi wa maeneo husika.

“Mradi unapowashirikisha wananchi mara zote nao huwa wana utunza, kuudhamini na kuulinda, hivyo nawapongeza RDO kwa kufanya uamuzi sahihi ya kubuni mradi huo pamoja na wananchi” amesema  Masenza.

Mkuu huyo wa mkoa wa Iringa amesema amesema mradi huo wa maji utatoa huduma kwa wananchi wengi na taasisi binafsi nyingi, hivyo jukumu la kila mwananchi kuutunza na kuuthamini ili udumu kwa muda mrefu.

“Nimesikia kwenye risala yenu kuwa mradi huu utahudumia kata za Ifwagi, Mdabulo, Ihanu, Luhunga, Mtitu na Kising’a na vijiji vya Igonongo, Ludilo, Kidete, Ikanga, Nandala, Ibwanzi, Isipii, Mkonge, Lulanzi, Luhindo, Barabara mbili na Isele.

“Hivyo ukiangalia utagundua kuwa mradi huu ni mkubwa na haupaswi kupuuzwa kwa kuwa unachochea maendeleo kwa wananchi wa maeneo ambayo umepita,” amesema.

Naye mkurugenzi mtendaji wa RDO, Fidelis Filipatali amesema mradi huo umegharimu sh.milioni 95,503,100 ambapo miongoni mwazo zipo fedha zilizochangwa na wananchi kwa ajili ya kufanikisha huduma hiyo.

“Sisi kama RDO ambao ndio wafadhili namba moja wa mradi huu wa maji tumechangia sh. 86,821,000 na wananchi 8,682,100,” amesema Filipatali

Filipatali amesema mradi huo utazalisha lita milioni 776 kwa vijiji vyote ambavyo vinatumia huduma hiyo inayonufaisha wananchi 10,874 na taasisi 18.

No comments:

Post a Comment