Friday, 2 March 2018

Rufaa ya Sugu Masonga kusikilizwa mahakama kuu
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mbeya, imepokea  rufani ya kupinga hukumu ya kifungo cha miezi mitano dhidi ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa Chadema kanda ya nyanda za juu kusini, Emmanuel Masonga.

Mmoja wa mawakili wa shauri hilo, Faraji Mangula amesema rufaa hiyo iliwasilishwa mahakamani hapo jana na kupewa kumbukumbu namba 29/2018.

Mangula amesema rufaa hiyo imeshapokelewa katika Mahakama Kuu na kwamba kinachosubiriwa ni kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa shauri hilo.

Amefafanua kuwa pamoja na mambo mengine yeye na wenzake (mawakili wa shauri hilo) wanakusudia kuomba dhamana dhidi ya wateja wao (Sugu na Masonga) ili wawe nje wakati rufaa yao inaendelea kusikilizwa.

Mangula ametanabaisha kuwa wateja (Mbilinyi na Masonga) walihukumiwa baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais Dk. John Magufuli ambapo walitoa kauli hiyo Desemba 30, mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge, jijini Mbeya.

No comments:

Post a Comment