Sunday, 18 March 2018

Samia achangisha milioni 700/-Samia Suluhu Hassan

SHILINGI milioni 700 zimepatikana katika harambee ya kuchangia ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Handeni. Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza harambee hiyo iliyofanyika hotel ya Golden Tulip wiki hii  Dar es Salaam.

Samia amewapongeza uongozi wa Wilaya ya Muheza na mkoa wa Tanga pamoja na wananchi kwa kuamua kujenga hospitali yao ya wilaya ili kuboresha hali ya afya na ustawi wa jamii.

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuimarisha ubora wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya vifo vya watoto kutoka kiwango cha vifo 66 kati ya vizazi hai 1,000 hadi kufikia kiwango cha angalau vifo 40 kati ya vizazi hai 1,000.

Aidha, Serikali imedhamiria kupunguza vifo vya wanawake wajawazito kutoka 556 kwa mwaka 2017 katika vizazi hai 100,000 hadi kufikia 292 ifikapo mwaka 2020.

Sanjari na hilo Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ina  mkakati wa kujenga, kukarabati na kupanua miundombinu ya vituo vya afya 208 ili kuimarisha utolewaji wa huduma mbalimbali za afya.

Makamu wa Rais ameutaka uongozi wa mkoa pamoja na wa wilaya ya Muheza kuupa kipaumbele mradi huu wa ujenzi na kuhakikisha bajeti inapokuja inawezesha ujenzi wa hospitali hiyo kukamilika kwa haraka.

Makamu wa Rais aliwashukuru wadau wote walioshiriki na kuomba kila mmoja achangie kwa uwezo na nafasi yake ili hospitali ya wilaya ya Muheza ikamilike mapema.

Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu amemshukuru makamu wa Rais kwa kuwezesha kufanikisha kupatikana kwa mchango huo mkubwaambapo aliahidi kuuenzi kwa kuhakikisha moja ya majengo linapewa jina la makamu wa rais.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi, Seleman Jafo pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto, Ummy Mwalimu.

No comments:

Post a Comment